27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RC MWANZA AJIPA SIKU 14 KUTATUA MADAI YA WALIMU


Na MASYENENE DAMIAN- MWANZA    |

WALIMU zaidi ya 400 waliohamishwa kutoka shule za sekondari kwenda msingi katika Jiji la Mwanza, wameandamana kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, John Mongella, kudai fedha za uhamisho.

Uamuzi wa walimu hao ulikuja baada ya jitihada mbalimbali za kufikia mwafaka na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, kugonga mwamba kutokana na kitendo chake cha kuweka askari nje ya ofisi zake kuwazuia wasimwone.

Baada ya kusikiliza madai ya walimu hao juzi katika ukumbi wa ofisi zake, Mongella, aliamua kutoa siku 14 kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mwanza, Kibamba, Ofisa Utumishi wa Jiji na wahusika wengine kujadiliana ili kuja na majibu na watakutana tena na walimu hao Mei 24, mwaka huu kujua mwafaka wao.

“Tupeane wiki mbili, sisi kwanza tumalizane humu ndani ndiyo tutakuja na maelezo, tutaonana Mei 24, mwaka huu saa moja na nusu asubuhi hapa hapa.

“Viongozi wa jiji hamuwezi kuja kunianika hapa kumbe mnajua mna makando kando yenu, hatutafika salama, inakuwaje mkurugenzi anajua kuna kesi kama hizi halafu ofisa utumishi hajui,” alisema.

Akizungumzia madai hayo, Mongella, aliwahakikishia kuwa watayapitia yote na hakuna hata mmoja mwenye haki atadhulumiwa, huku akiwakumbusha kufuata utaratibu wanapodai stahiki zao ikiwamo kutoa taarifa kwa mwajiri wao juu ya kutoonekana katika vituo vya kazi.

“Wapo wenye sifa za kulipwa, wapo ambao hawastahili chochote na kinachosema hii ni sheria, tutafuata utaratibu ili mwenye haki asiipoteze na tunafuata sheria ili maagizo ya viongozi wetu yasitafsiriwe tofauti.

“Kwa hili hapa ndugu zangu siwezi kuwapa majibu ya mkato ya kuwafurahisha, kama kuna mtu ana hoja ya msingi tutamsikiliza na katika hili hakuna haki ya mtu itakayopotea,” alisema.

Awali wakizungumzia kilichowasukuma kuonana na Mongella, baadhi ya walimu walisema kumekuwa na harufu ya rushwa katika stahiki zao za uhamisho baada ya Kibamba kusema watalipwa kulingana na umbali wa kilomita za shule walikopelekwa.

Mwalimu Martin Kisambale, aliyehamishwa kutoka Shule ya Msingi Lake kwenda Nyanshana pamoja na wenzake watano, lakini wenzake wamelipwa lakini yeye bado.

“Katika madai yetu haya zaidi ya walimu 200 waliohamishwa wenzetu 30 wamelipwa na mkurugenzi alipita kila shule kutuaminisha tuandike barua kuomba tulipwe fedha kwa sababu zipo lakini leo (jana) ametugeuka anasema hatulipwi na hatuna vigezo,” alisema.

Naye Mwalimu Mariam Mashauri wa Shule ya Msingi Mirongo, alisema kikubwa wanachokidai ni fedha za uhamisho baada ya kuhamishwa mapema mwaka huu na kuahidiwa kuwa fedha zao zipo lakini baadaye alikuja kuwaambia kuwa watalipwa Sh 200,000 za motisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles