Susan Uhinga, Tanga
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ukiongozwa na Waziri wa Mafuta wa nchi hiyo Ngoi Mukena wamefika Mkoani Tanga, kujionea Uboreshwaji wa miundombinu ya Bandari  na wa ya kampuni ya GBP ambao ni waingizaji wa mafuta nchini.
Akizungumza na waandishi wa Habari waziri huyo amesema amefurahishwa na miundombinu ya kisasa katika kampuni ya GBP pamoja na uboreshwaji wa Bandari ya Tanga.
” Nimefurahishwa na kwa hakika sasa tunaona umuhimu wa kutumia bandari ya Tanga kuchukua mafuta na kuyaleta nchini kwetu niseme nimeridhishwa” amesema.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Bandari Mkoani Tanga Donald Ngaile amesema kwa sasa mchakato wa upanuzi wa bandari ya Tanga unaendelea na tayari upimaji wa miamba iliyoko chini ya bahari umeshafanyika.
“Kwa sasa Bandari yetu ina uwezo wa kuhudumia hata nchi za jirani hivyo tunawakaribisha wenzetu wa Congo watumie bandari yetu kwani tuna uwezo wa kuwahudumia vizuri na kwa wakati” amesema.
Naye Muwekezaji wa Kampuni ya uingizaji wa mafuta Nchini (GBP), Sudi Badar ameishukuru serikali ya Rais Magufuli kwa kusimamia mifumo mizuri ya uwekezaji ambayo itawezesha kampuni kuhudumia na nchi jirani na Tanzania.