25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI, WB ZAJADILI MKOPO KUPUNGUZA MAFURIKO BONDE LA MSIMBAZI

Na Aziza Masoud – Dar es Salaam                     |              


SERIKALI inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia (WB) kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 60 (Sh bilioni 137.2) za utekelezaji wa mradi wa Bonde la Mto Msimbazi ili kumaliza tatizo la mafuriko na uharibifu wa miundombinu unaojitokeza wakati wa mvua.

Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara ya wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (LAAC) iliyokusudia kukagua miradi ya uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema mkopo wa fedha hizo ni kati ya dola milioni 80 zinazohitajika ili kutekeleza mradi huo.

“Kati ya Dola za Marekani milioni 80 (Sh bilioni 182.2) zinazohitajika, Serikali tayari tumeshapata dola milioni 20 (Sh bilioni 45). Katika mazungumzo yanayoendelea na Benki ya Dunia, tukipata dola milioni 60 (Sh bilioni 137.2 ), ndoto zetu tutaweza kuziendeleza na kulifanya eneo la Mto Msimbazi kuwa kivutio cha utalii badala ya kuwa kero kwa wananchi,” alisema Jafo.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kumeshirikisha watu zaidi ya 1,000 na utawezesha magari kupita muda wote hata kipindi cha mvua.

Jafo alisema kukamilika kwa mradi huo pia kutatatua tatizo la magari ya mwendokasi kushindwa kutoa huduma kipindi cha mvua na jukumu lao kama viongozi ni kufanya uamuzi sahihi.

“Matamanio yetu ni kwamba kabla Serikali haijaondoka madarakani, ndoto za mradi huu ziwe zimetimia na tunaamini italeta matokeo makubwa, tunatamani jambo hili mwakani liingie katika bajeti yetu,” alisema.

Alisema mradi huo utaokoa maisha ya watu wanaopata shida ya mafuriko kipindi cha mvua, pia ni wa uwekezaji na utakuwa kivutio cha watalii.

Mmoja wa wajumbe wa LAAC ambaye pia ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alipongeza jitihada hizo za Serikali na kuiomba kuweka utaratibu maalumu wa usimamizi wa miradi hiyo iliyogharimu fedha nyingi.

Pia kamati hiyo ilitembelea mradi wa barabara ya kilomita 3.3 kutoka Tuangoma hadi Mbagala Kuu, iliyojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 12 na mradi wa ujenzi wa Soko la Kijichi linalojengwa kwa Sh milioni 700.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles