Mwandishi Wetu -Dodoma
SERIKALI na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), wameandaa mfumo wa kieletroniki wa kuwasilisha taarifa, ikiwamo malalamiko, maoni na kupata mrejesho ili kuinua daraja wa uwekezaji nchini na kuzidi kuboresha mazingira ya kufanya biashara ambao utaanza kutumika mwaka 2020/2021.
Akitangaza ubunifu huo jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2020/2021, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisifu mfumo huo na kusema kwamba utapunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wawekezaji na kulieleza Bunge kwamba juhudi ya Watanzania kujiletea maendeleo ya kisasa inazaa matunda.
“Mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara vimeendelea kuimarika, na ushahidi huu inathibitishwa na taarifa ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia juu ya Wepesi wa kufanya Biashara ya mwaka 2020. Tanzania imepanda kwa nafasi tatu kutoka nafasi ya 144 hadi nafasi ya 141,’’ alisema Majaliwa
Licha ya hali hiyo aliliambia Bunge kwamba mfumo huo wa kieletroki utaoneza ufanisi zaidi katika ukuzaji uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.
Aliahidi kwamba serikali ikishirikiana na TPSF itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara ili kupata nafasi za juu ya dunia katika eneo hili. biashara.
Waziri Mkuu amezitaka taaasisi zote za serikali kuweka mazingira mazuri na rafiki kwa uwekezaji, kuimarisha uratibu wa ukaribu na kufungua fursa zaidi za uwekezaji na ufanyaji biashara.
“Serikali itaendelea kuhamasisha mikoa yote nchini kuandaa makongamano ya uwekezaji na kuzindua miongozo ya uwekezaji ya mikoa inayobainisha fursa za uwekezaji ili kufikia nafasi ya juu ya utendaji ifikapo mwaka 2025,’’ alisema
Waziri Mkuu alisema kuwa serikali itahakikisha maeneo ya uwekezaji yanatengwa na kuendelezwa kwa kuwekewa miundombinu ya msingi .
“Juhudi kubwa imefanywa na serikali za mikoa kwa kuzindua miongozo ya fursa za kiuwekezaji ambapo jumla ya hekta 854,821 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo halmashauri zote nchini,’’ alisema