Na Dinna Maningo,Tarime
VIONGOZI wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilaya ya Tarime, wamemtaka mkuu wa mkoa wa Mara, Ally Hapi kuacha kuwatuhumu kuwa wamehusika katika wizi wa fedha za miradi ya jamii inayojengwa kwa fedha za Uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR).
Wamesema kuwa waliohusika kujenga miradi kupitia mafundi loko,kutoa fedha za malipo, manunuzi ya vifaa na zabuni ni ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo, wataalamu wa halmashauri huku mgodi ukiwa ndiyo mtoa fedha kwenda kwenye halmashauri kisha kulipa fedha za miradi ya ujenzi.
Wakitoa malalamiko yao mbele ya Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara, Aprili 24, 2022 katika ukumbi wa shule ya sekondari Ingwe, Mwenyekiti wa kamati ya mendeleo ya jamii (CDC) katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi, Paul Bageni amesema kuwa RC Hapi kawatwisha mzigo usio wahusu huku wausika ambao ni serikali ya Tarime akiwafumbia macho licha yakwamba wao hawajawahi kushirikishwa kwenye matumizi ya fedha zaidi ya kutoa vipaumbele vilivyoibuliwa na vijiji pamoja na usimamizi wa miradi.
“CDC ilianzishwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Tarime Glorius Luoga mwaka 2017 lengo likiwa ni kuunganisha mgodi na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya jamii kwenye vijiji vinavyozunguka na mgodi,baada ya kuanzishwa alikaa muda mfupi akaondoka akaja Charles Kabeho nae alikaa muda mfupi akaondoka na wote tulikaa nao vikao vya kujadili vipaumbele na kupanga matumizi ya fedha.
“2019-2020 aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Tarime, Mtemi Msafiri wakati wa kipindi chake ndiyo manunuzi yalifanyika yeye ndiye alivuruga mambo vikao vingine hakutushirikisha CDC alivifanyia ofisini kwake, tulikaa nae baadhi ya vikao tukiwa na katibu tawala wa wilaya, John Marwa,na wataalamu mbalimbali wa halmashauri na aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri Apoo Tindwa.
“Kazi yetu CDC ilikuwa nikuwasilisha vipaumbele vya miradi ya vijiji tunapanga gharama za miradi tunajadili fedha zilizopatikana kwa kila Kijiji je zitatosha? kisha halmashauri kupitia wataalamu wanasanifu na kuangalia mradi ulioibuliwa utakidhi gharama za fedha? wao ndiyo watafuta mafundi na wafanya manunuzi sisi ni kusimamia mradi tu mambo yote ya kitaalamu waliwajibika wao,” alisema Bageni.
Aliongeza kusema kuwa CDC ina wajumbe mbalimbali wakiwemo Wenyeviti wa vijiji, TAKUKURU, watendaji wa vijiji na kata,afisa mahusiano wa mgodi akitambulika kama katibu kwakuwa ndiyo alikuwa mtoa fedha za CSR, mkuu wa wilaya, katibu tawala wa wilaya,mkurugenzi wa halmashauri, Madiwani, Jamii, viongozi wa dini,na wataalamu wa idara mbalimbali kama afya, elimu, maji na idara ya maendeleo ya jamii nakwamba CDC haikuwa na ofisi ila walikutana na kukaa vikao vyote ambapo katibu alisoma mhitasari wa kikao kilichopita waliporidhia waliendelea na kikao.
Bageni alisema kuwa yuko tayali kukamatwa kwakuwa anaamini hajahusika katika ubadhilifu wowote wa fedha za CSR nakwamba RC Hapi alifanya makosa kuwatuhumu na kutoa maamuzi bila kuwapa nafasi kuwasikiliza licha yakwamba halmashauri ndiyo inayolipa fedha za miradi yote ya CSR baada ya kupokea kutoka mgodini.
“Mimi ndiyo natuhumiwa mbali na kuwa Mwenyekiti wa CDC ni mwenyekiti wa Kijiji cha mjini kati ,kila tunachokifanya tunashirikisha serikali, RC anasema CDC tunajiamlia wenyewe hapana!vijiji ndiyo vinaibua vipaumbele vinapeleka kwenye mkutano mkuu wanabariki,WDC inapitia inachakata alafu CDC nayo inapitia alafu inaenda halmashauri ya wilaya ambako huko ndiyo kuna wataalamu wa kila idara nao wanachakata wanasanifu na kutoa ushauri kulingana na mradi kujua kiasi kinachohitajika ni kadhaa.
“Baada ya hapo halmashauri inatangaza tenda kujenga miradi mgodi unalipa kupitia halmashauri,naomba nikamatwe ili nitoe maelezo yakutosha RC awe anatoa maamuzi kwa kusikiliza pande zote yeye ni kiongozi mkubwa tunamuheshimu hebu atupe nafasi na sisi watu wa chini, hakuna sehemu yoyote niliyowahi kusaini fedha za miradi mimi ni kuibua na kusimamia, wataalamu ndiyo walihusika kuhidhinisha gharama za miradi na halmashauri inalipa fedha baada ya kupokea kutoka mgodini,” alisema Bageni.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyangoto Mwita Msegi alisema kuwa vijiji viliibua miradi na kuipeleka CDC kama kiungo kinachojumuisha miradi yote ya vijiji na kupeleka halmashauri nayo inachakata kupitia wataalamu wake wanapanga bei kisha CMT nayo inapitia inatuma mkoani nao wanatuma TAMISEMI wakipitia wanarudisha mkoani na mkoa unarudisha wilayani ambapo watekelezaji ni halmashauri.
“Watekelezaji wa miradi yote ya CSR ni Serikali tuna kamati ya CDC na za vijiji lakini hatujawahi kushirikishwa kwenye manunuzi,sisi vijiji tulipewa kazi ya kusimamia ujenzi wa miradi kamati za vijiji waliokuwa wanasimamia walilipwa posho 10,000 humohumo na nauli kwa bahati mbaya aliyekuwa afisa mipango akifariki yeye ndiyo alikuwa anajua kila kitu hata baadhi ya vitu alikuwa akishinikizwa kwa nguvu bila hiari yake,” alisema Msegi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kerende Mniko Magabe alisema kuwa malipo ya posho za vikao zilitofautiana kulingana na umbali wa kijiji husika waliofika kufanya kikao katika kijiji cha mjini kati ambapo malipo yalikuwa kati ya 5,000-15000 ambazo ni malipo ya posho na nauli zilizolipwa na halmashauri ya wilaya ya Tarime.
Diwani wa kata ya Matongo, Godfrey Kegoye alisema kuwa mgodi huo ulisimamisha utoaji wa fedha za CSR tangu 2020-2022 na serikali ya Mara kwa madai ya kufanya uchunguzi kutokana na kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha kwenye miradi licha yakwamba CDC siyo mtoaji wa fedha yeye ni muibuaji wa vipaumbele kisha vinapelekwa halmashauri mgodi unatoa fedha halmashauri inalipa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Kemambo, Rashid Kisiri alisema kuwa wananchi wa Nyamongo hawajui CDC nakwamba kauli ya RC Hapi kusema CDC ni wezi wanakula fedha za wanyamongo ilileta taharuki nakwamba CDC ni chombo kikubwa chenye wajumbe wengi lakini halmashauri na serikali ya Tarime ndiyo wanaojua matumizi ya fedha za miradi.
“Hili suala la fedha za CSR tulifanyie Kazi vinginevyo litatugawa wanaposema ni majizi bila kufafanua unaiweka CCM kwenye wakati mgumu hata kwenye chaguzi itatusumbua unamtuhumu mtu mtaje jina lake usiunganishe watu wote,viongozi wasitoe tuhuma kabla ya kujiridhisha,” alisema.
Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara alisema kuwa CDC siyo watoa fedha bali ni waibuaji wa miradi, madiwani wanaipangia mipango halmashauri inatekeleza na miradi yote imesainiwa na aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa, tumechaguliwa 2020 tumeanza kazi mwaka 2022 mgodi umetoa fedha Sh bilioni 5.6 lakini RC Hapi kazuia miradi imesimama hakuna fedha.
“Kuvunjwa kwa CDC mimi naona ni sawa kwasababu ilikuwepo lakini hatujaona umuhimu wake kwakuwa wajumbe hawashirikishwi vyakutosha kwenye miradi hata kwenye kikao cha RC hata mimi mbunge hakunipa nafasi nizungumze huwezi kumuhukumu mtu bila kusikiliza,Milioni 167 za mikopo ya vijana,wanawake na walemavu zimepigwa,” alisema Waitara.
April 20,2022 katika kikao cha wadau wa Mendeleo kilichofanyika mjini Musoma, Mkuu wa mkoa wa Mara, Ally Hapi alivunja kamati ya CDC ambayo alidai ilikuwa inapanga matumizi ya fedha za miradi za CSR na kuhusika katika matumizi mabaya ya fedha za miradi na kuviagiza vyombo vya dora husuani jeshi la polisi mkoa wa polisi Tarime/Rorya, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU na vyombo vingine kuwafungulia majalada ya uchunguzi viongozi wa CDC.
Hapi alisema kuwa sababu ya kuivunja ni kutokana na CDC kuhusika kwenye matumizi mabaya ya fedha za CSR ambayo haina mguu wa sheria nakwamba imekuwa ikipanga matumizi ya miradi ya kijamii bila kushirikisha wataalamu husika wala wananchi walengwa na imekuwa ikiamua hadi miradi ya maji,afya na elimu wakati haina wataalamu.
“Mwenyekiti na katibu wa CDC kuanzia sasa biashara ya CDC imekufa na mkawaambie wajumbe wale 200 wakatafute kazi za kufanya,ripoti ninayo walikuwa wakienda kupanga matumizi ya fedha ripoti hii ni ya 2018-2020Meneja mkuu wa mgodi fanya mabadiliko ya Meneja uhusiano hatuko tayali kufanya nae Kazi .
Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara na kuhamishiwa mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robart Gabriel aliunda kamati ya kuchunguza fedha za CSR zilizotumika kwenye miradi kwa kipindi cha 2018-2020 na ripoti hiyo kukabidhiwa kwa mkuu wa mkoa wa Mara Ally Hapi ambaye amevitaka vyombo vya dora kuwafungulia majalada ya uchunguzi viongozi wezi wa fedha za miradi.