Na Hadia Khamis, Mtanzania Digital
BARAZA la Mawaziri linatarajia kuwasilisha mswada wa sheria itakayolinda taarifa binafsi za kimtandao.
Muswada huo utapekekwa bungeni kesho Septemba 13, mwaka huu kwa ajili ya kusomwa kwa mara yakwanza na baada ya hapo utaanza kujadiliwa.
Akizungumza juzi Dar es Salaam katika kongamano la kuwaunganisha wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Waziri wa TEHAMA Nape Nnauye alisema kuwepo kwa sheria hiyo itasaidia taarifa za watu binafsi zisitoke nje.
Amesema baada ya muswada huo washeria kupelekwa bungeni na kila mdau atatakiwa kutoa maoni yake ili kuweza kukamilisha sheria hiyo.
“Baraza la Mawaziri tumeshaanda sheria ya muswada huo ili kuondoa kabisa tatizo la baadhi ya watu wanaotumia vibaya mitandao,” amesema Nape.
Pia Nape amefafanua kuwa kongamano hilo la siku mbili litaelimisha mambo mbalimbali ya TEHAMA kwa kuwa limewaunganisha wadau sekta hiyo wakiwemo wa miundombinu wa ndani na nje ya nchi.
“Lengo la Serikali halitaki kumuacha nyuma mtanzania kwa kuwa teknolojia ya kisasa itasaidia mambo mengi ikiwemo kwenye ajira na hata kupata wawekezaji wengi,” amesema Nape.