28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kutoa ubani kwa wafiwa wa tetemeko Bukoba

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto), akipokea hundi ya Sh milioni 100 kutoka kwa Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Caspian, Omid Karambeck, mjini Dodoma jana kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto), akipokea hundi ya Sh milioni 100 kutoka kwa Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Caspian, Omid Karambeck, mjini Dodoma jana kwa ajili ya waathirika wa
tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Na MAREGESI PAUL, DODOMA

SERIKALI imesema itatoa fidia ya Sh milioni 1.17 kwa kila familia iliyofiwa na ndugu wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu mkoani Kagera.

Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa nne wa Bunge la 11.

“Kama Bunge lako tukufu lilivyojulishwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imechukua hatua kadhaa kushughulikia athari za tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu.

“Pamoja na viongozi kutembelea maeneo yenye madhara, Serikali pia imewapatia chakula waathirika, imeimarisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa kupeleka dawa na vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa na pia imepeleka timu ya wataalamu na madaktari 12 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

“Wananchi waliokosa kabisa hifadhi ya makazi, wamepewa maturubai na mahema kwa ajili ya makazi ya muda na waathirika ambao nyumba zao zimebomoka kabisa kwa kuanzia kila mmoja ametengewa mabati 20, saruji mifuko mitano pamoja na mablanketi na mikeka na kwa wapangaji waliokuwa katika nyumba hizo kila mmoja ametengewa kodi ya pango ya miezi sita ili apate mahali pa kujihifadhi.

“Tathmini ya uharibifu wa barabara imefanyika na barabara zilizoharibika zitarejeshwa katika hali yake ya kawaida ili wananchi waendelee kupata huduma za msingi huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kukarabati miundombinu ya maji safi na maji taka.

“Pamoja na hayo, Serikali imewafariji wafiwa na kushiriki mazishi kwa kusaidia kutoa majeneza, sanda, usafiri na kutenga shilingi milioni 20 za rambirambi kwa wafiwa ambazo zitatolewa kwao muda wowote,” alisema Majaliwa.

Pia alizungumzia mwenendo wa ukusanyaji wa mapato serikalini na kusema Serikali imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji huo kwa kuchukua hatua mbalimbali.

Katika hatua nyingine, alisema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, mapato ya Serikali yanatarajia kuongezeka na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka kwa washirika wa maendeleo huku ikiendelea kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi ili kuleta tija kwa Taifa.

“Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali imelenga kukusanya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri ya jumla ya shilingi trilioni 18.46. Takwimu za mwenendo wa ukusanyaji wa mapato zinaonyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Agosti, mwaka huu, mapato yaliyokusanywa na TRA yalikuwa shilingi trilioni 2.168 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles