Leonard Mang’oha-Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye ulemavu, Jenista Mhagama, amesema kuanzia sasa mafuta ya kukinga ngozi na miale ya jua kwa albino, yataagizwa pamoja na dawa nyingine kuhakikisha yanapatikana kwa urahisi nchini.
Mhagama alitoa kauli hiyo katika hafla ya kupokea na kukabidhi mashine za kuchapisha maandishi ya nukta nundu jana, vilivyotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa ajili ya watu wenye ulemavu, katika kwa shule na vyuo mbalimbali nchini.
Mhagama alizitaka taasisi za umma, binafsi na mashirika mbalimbali kutambua kuwa zina nafasi kubwa ya kufanikisha malengo ya watu wenye ulemavu.
“Taasisi zinapokwenda kutoa fedha za kusaidia jamii ziwe taasisi za umma, binafsi au mashirika ziwe zinaangalia na vifaa vya watu wenye ulemavu.
“Mnaweza kujiuliza kwamba kwa nini tumekuja hapa waziri na Naibu Waziri.
“Watu wenye ulemavu ni nguvukazi katika taifa, wanapaswa kuheshimiwa kama wanavyoheshimiwa wengine, kuwa na ulemavu hakuwazuii kujumuishwa katika shughuli mbalimbali.
“Mkiendelea kuwabagua katika elimu, ajira, biashara na mambo mengine ni kuwanyima haki,” alisema Jenista.
Naye Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Masha Mshomba, alisema vifaa hivyo ni utekelezaji wa ahadi waliyoitoa katika mkutano mkuu wa mwaka uliopita.
“Mtakumbukaa tulifanya mkutano wetu mkuu wa mwaka kule Arusha na tuliahidi kusaidia watu wenye ulemavu na tulisema tutasaidia kununua mashine za nukta nundu, kwa hiyo tupo hapa kutekeleza hilo,” alisema Mshomba.
Alisema mashine zilizotolewa ni 13 ambazo zitasaidia kuongeza ufanisi katika kujifunza na kuwawezesha wanufaika kuwa washindani katika soko la ajira.
“Hiki ni kipaumbele chetu na tutafurahi zaidi kwa kupanua zaidi huduma zetu kwa wananchi,” alisema Mshomba.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia wenye ulemavu, Stella Ikupa, aliwataka wanafunzi hao wenye ulemavu kujikubali, kujithamini na kujitambua.
Alisema hakuna anayeweza kuwatambua kama hawatafanya hivyo wao wenyewe.
Alisema vifaa hivyo ni muhimu kwa watu wenye ulemavu wa macho kwa sababu vitawawezesha kujumuishwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo elimu.
Aliziomba taasisi mbalimbali za umma na binafsi kuendelea kujitolea kusaidia makundi ya watu wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu.