Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
SERIKALI inakusudia kupanua huduma za matibabu ya dharura katika
Hospitali ya Kanda Mbeya na Hospitali ya Mount Meru, ili kuboresha
huduma za matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa dharura.
Kwa sasa hospitali pekee yenye idara maalumu inayotoa huduma ya
matibabu ya dharura nchini ni Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu – Afya wa Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubsya,
alipokuwa akizindua Kongamano Kuu la
pili la Watoa Huduma za Tiba ya Dharura na Kuokoa Maisha.
“Kihistoria nchini mwetu, Hospitali ya Taifa Muhimbili ndiyo pekee ambayo ina idara maalumu kwa ajili ya kutoa huduma za dharura kwa watu wanaohitaji huduma hiyo kuokoa maisha yao,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imepanga kupanua wigo wa
huduma hiyo katika maeneo mengine kwa kuanzia na Hospitali ya Kanda
Mbeya na Mount Meru.
“Tunakusudia pia huduma hizi zianze kutolewa hadi katika hospitali
binafsi kisha tutaendelea hadi katika hospitali za rufaa za mikoa na
wilaya,” alisema na kuongeza:
“Kinachoendelea sasa ni kuwapa mafunzo wataalamu
ili kuongeza idadi yao, tunao 27 na hivi karibuni kuna ambao
watahitimu mafunzo na hivyo idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia
wataalamu 36.
Alisema barani Afrika tafiti zinaonesha asilimia 40 ya watu hufariki
dunia kutokana na kucheleweshwa kufikishwa hospitalini pale
inapohitajika huduma za dharura.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hilo, Dk. Upendo
George, alisema jumla ya wataalamu 250 wamepatiwa mafunzo kuongeza
ujuzi wao.
“Mafunzo hayo yalifanyika kabla ya kuja kwenye kongamano hili na
tumewapa mbinu ambazo wanaweza kuzitumia hata kwa kutumia vifaa
vichache walivyonavyo kuweza kuokoa maisha,” alisema.