Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
Serikali inatarajia kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa wanaomiliki makampuni nje ya nchi baada ya watalaamu wa kodi kutoka Chuo Cha Kodi nchini (ITA) kufanya utafiti mwaka 2017/18 wa kuangalia mfumo unaoweza kuisaidia serikali kupata mapato.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Novemba 15, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Isaya Jairo, amesema mfumo huo unayojulikana kwa jina la (High Network Individual) utaweza kuwafikia wafanyabiashara hao katika ulipaji wa kodi.
“Lakini pia utaweza kumfikia mtu mmoja mmoja ili kuhakikisha analipa kodi stahiki za serikali, jambo ambalo linaweza kusaidia kuongeza mapato,” amesema.
Aidha, amesema mara baada ya kuanza kutumika kwa mfumo huo wataweza kutatua changamoto za ukusanyaji wa kodi kupitia kada hiyo, jambo ambalo linaweza kuisaidia serikali kupata mapato kupitia mfumo huo.
“Tulifanya utafiti ili tuweze kubaini suluhisho la ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara wakubwa wanaomiliki biashara nje ya nchi, jambo ambalo limetufanya tuje na mfumo unaojulikana’ High Network Individual’ ambao utaweza kumfikia mtu mmoja mmoja kulingana na nafasi yake,” amesema Jairo.