24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Utafiti: Hakuna shida wanawake kulea mwaka mimba mwaka mtoto

JOSEPH HIZA NA MTANDAOUTAFITI mpya umebainisha kwamba akina mama wanapaswa kusubiri kwa mwaka mmoja tu baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine ili kupunguza hatari ya kumpoteza mama na mtoto.

Kwa msingi huo, watafiti hao wanaamaanisha kwamba hakuna ulazima wa wanawake kusubiri kwa muda wa miezi 18 kama ilivyopendekezwa katika kanuni iliyopo sasa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kabla ya ujauzito mwingine.

Muda mfupi kati ya mimba moja hadi nyingine humuweka mama katika hatari ya kuzaa mtoto ambaye hajatimiza muda wa kuzaliwa, mtoto kuwa na uzito mdogo au kusababisha kifo chake.

Watafiti wana matumaini kuwa matokeo ya uchunguzi huu utawapatia hakikisho wanawake wenye umri mkubwa, ambao huwa katika shinikizo wakati wanapojaribu kutunga mimba nyingine kabla ya muda wao wa kuzaa kupita kutokana na umri wao.

Mmoja wa watafiti hao, Dk. Wendy Norman, anasema hizi ni habari njema kwa wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 35 ambao wanapanga familia zao.

“Wanawake walio na umri mkubwa kwa mara ya kwanza watapata mwongozo wa uhakika kuhusiana na suala la kupanga uzazi wa watoto wao,” anasema katika utafiti huo uliochapishwa na Jarida la JAMA Internal Medicine.

Utafiti uliohusisha kuzaliwa kwa karibu watoto 150,000 nchini Canada, uliofanywa na vyuo vikuu vya British Columbia (UBC) na Harvard cha nchini Marekani, umebaini kuwa miezi 12 hadi 18 ni muda mwafaka kwa mwanamke kujipumzisha baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine.

Mwongozo wa sasa wa WHO unapendekeza muda usiopungua miezi 18 hadi 24.

Wanawake wadogo waliopata ujauzito miezi sita baada ya kujifungua walikua katika hatari ya kupata uchungu wa uzazi kabla ya muda wa kujifungua kwa asilimia 8.5.

Hali hii inaweza kupunguzwa kwa hadi asilimia 3.7 iwapo wanawake hao wangesubiri kwa miezi 18 kati ya ujauzito mmoja hadi mwingine.

Utafiti huo uliangazia zaidi wanawake nchini Canada hivyo, haijabainika ikiwa matokeo yake yatakuwa sawa kote duniani.

Mtafiti Dk. Sonia Hernandez-Diaz, anasema matokeo hayo yaliashiria hali tofauti kwa wanawake wa miaka tofauti.

“Ujauzito wa haraka haraka huenda ukaashiria kutozingatia uzazi wa mpango, kwa baadhi ya wanawake wenye umri mdogo.

Mandy Forrester, kutoka taasisi ya wakunga ya Royal College, anasema utafiti huu ni muhimu kwa sababu unaimarisha tafiti nyingine kuhusu suala la muda wa kupata ujauzito mwingine baada ya kujifungua.

“Yote tisa, kumi ni kwamba mwanamke atajiamulia mwenyewe anataka kuchukua muda gani baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine.”

Anasema jambo la msingi ni kwa wanawake kote duniani kuwa na ufahamu wa kujihami nao kuhusiana na suala hili ili wafanye uamuzi wa busara.

“Wataalamu wa afya wako tayari kumsaidia mwanamke kufanya uamuzi kuhusiana na kile kilicho sawa kwake,” anasema.

Anaongeza kuwa wanawake wanastahili kupata ushauri kuhusu mbinu tofauti za kupanga uzazi ili waweze kupanga familia zao ikiwa wanaazimia kufanya hivyo.

“Huduma za kitaalamu zinastahili kufikia wanawake wote,” anasema.

Dk. Laura Gaudet, mtaalamu wa afya katika Hospitali ya Ottawa nchini Canada, anasema wengi wa wanawake wanaofika hospitalini hapo kwa huduma za uzazi ni wanawake wenye umri wa miaka zaidi ya 35.”

Wako katikati ya mihangaiko mingine ikiwamo kimasomo na bado wanataka kuzaa siku moja na wanajiuliza nini watafanya watakapofikisha miaka 35 kabla ya kufanikisha ndoto hiyo. “Ni swali linaloulizwa sana na ambalo nakutana nalo,” anasema mtaalamu huyo wa uzazi ambaye pia anafundisha katika Chuo Kikuu cha Ottawa-Tiba ya Uzazi.

Kwa mujibu wa Chama cha Wakunga nchini Canada, zaidi ya nusu ya uzazi nchini humo hutokana na wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 30.

Nchini humo na kwingineko duniani, aina ya maisha tunayoishi kila siku, mambo ya kutafuta elimu, ajira, kutafuta wapenzi waaminifu, hizi zote zimekuwa ni miongoni mwa sababu za wanawake wengi kujikuta wanatafuta ujauzito au watoto huku wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 35.

Kwa mujibu wa tafiti za awali, mwanamke kuwa mjamzito akiwa na umri wa miaka zaidi ya 35, kuna athari si tu kwa mjamzito, bali pia hata kwa mtoto atakayezaliwa.

Inaelezwa kuwa katika ukuaji na kukomaa kwa mwili wa mwanamke, ili aweze kupata ujauzito na baadaye kujifungua salama, mtoto mwenye hali nzuri kiafya, inawezeshwa na mabadiliko ya kibaiolojia ndani ya mwili wa mwanamke.

Mabadiliko haya huletwa na kemikali asilia ndani ya mwili ambazo kitaalamu huitwa hormone.

Mwanamke anapokuwa amepevuka, mwili wake huwa na kiwango kikubwa cha homoni ambazo humuwezesha kupata mabadiliko muhimu ya kimwili yanayomtambulisha au kumfanya awe na sifa au tabia halisi za mwanamke.

Kitaalamu homoni hizi kwa mwanamke, uzalishwaji wake mwilini na namna zinavyofanya kazi huwa zina muda maalumu au kikomo cha kutengenezwa mwilini, au hata kama zitatengenezwa basi hazitakuwa katika kiwango cha kutosha na hivyo kumfanya mwanamke kutoyaona baadhi ya mabadiliko ya kimwili ambayo alikuwa akiyaona pindi alipokuwa kijana na hasa chini ya miaka 35.

Athari zinazoweza kujitokeza kwa mwanamke kupata ujauzito akiwa na umri wa zaidi ya miaka 35 ni pamoja ugumu na unadra wa kupata ujauzito, kutokana na mayai kutozalishwa mwilini mwake.

Na kama ikitokea akapata ujauzito, mwanamke atakuwa hatarini kupoteza ujauzito wake kutokana na kupungua kwa uwezo wake wa kustahimili na hivyo mimba kutoka.

Endapo atastahimili kuwa mjamzito katika umri huo, zaidi ya miaka 35, kuna hatari ya mwanamke kupata maumivu makali zaidi wakati wa kujifungua, hii inasababishwa na kupungua kwa uwezo wa kumsukuma mtoto, shingo ya kizazi kushindwa kufunguka vizuri na pia mtoto kutotoka vizuri. Kutokana na tatizo hili, mwanamke huweza kujikuta akifanyiwa upasuaji ili kuweza kumsaidia ajifungue vizuri.

Kwa upande wa mtoto, athari anazoweza kuzipata ni pamoja na hizi zifuatazo:

Mtoto huwa katika hatari ya kuzaliwa akiwa na ulemavu, mfano, matatizo ya kushindwa kuongea vizuri (ulimi mzito), matatizo ya akili (mtindio wa ubongo), matatizo ya uti wa mgongo, pia matatizo katika viungo vingine mwilini kama mikono na miguu, kitaalamu tatizo hili huitwa, Down’s Syndrome.

Hii husababishwa na mtoto kukosa vitu muhimu wakati alipokuwa tumboni mwa mama yake, na mama yake hakuwa na vitu hivyo (homoni) kutokana na umri wake kuwa mkubwa zaidi.

Kwa sababu hizo, wanawake wengi husikia kwamba mwisho wa uzazi kwa wanawake ni baada ya miaka 35 na hatari ya matatizo ya mimba huongezeka.

Na ni kweli kwamba mambo haya hutokea wakati mtu anapozidi kuwa na umri mkubwa — lakini hauhusishi mwaka kamili.

Kuna wengine hujifungua bila matatizo na baadhi ya watafiti hutofautiana kuhusu umri, wakisema isiwe kigezo cha kuzuia wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35 kujifungua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles