25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kuja na Mkakati wa Kitaifa kuhusu Nishati Jadidifu, TaTEDO watia neno

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

SERIKALI ipo katika maandalizi ya kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamebainishwa na hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda, katika warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania(TaTEDO).

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda.

Amesema serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu kupitia Wizara ya Nishati ili kuongeza mchango wa Nishati Jadidifu katika upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.

Kwa mujibu wa Nyanda, Nishati Jadidifu ni vyanzo vya kuzalisha umeme visivyoisha ikiwemo upepo, jua, joto ardhi, mawimbi ya bahari, maporomoko ya maji ambayo ni chini ya megawati 10 na vingine ambavyo vinauwezo wa kuzalisha nishati bila kuchafua mazingira.

“Kupitia Sera yake ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 serikali inaweka kipaumbele katika uendelezaji wa rasilimali za nishati jadidifu kwa kuwa ni rasilimali endelevu na nyingi zinapatikana hapa nchini.

“Katika sekta ya Nishati ukitaka upunguze athari za mabadiliko ya tabia nchi ni lazima utumie nishati jadidifu na matumizi bora ya nishati.

“Sera yetu inatambua nishati jadidifu lakini na sera zingine kama ya Mazingira ya Mwaka 2021 na Mkakati wa Kitaita wa Mazingira ambazo zote hizo ni muendelezo wa nishati jadidifu,” amesema Nyanda.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mkakati huo kutatoa muongozo mzuri wa uendelezaji wa nishati jadidifu hapa nchini.

“Mpango wa sasa wa wizara nikuandaa mkakati wa kitaifa wa Nishati Jadidifu na tupo katika hatua nzuri na tayari mshauri elekezi ameshaanza maandalizi ya mkakati na kwa sasa anaendelea kupata maoni ya wadau hadi mwakani mwezi wa pili itakuwa imekamilika.

“Hivyo wanahabari mnao wajibu wa kutusaidia kutoa elimu ya umuhimu wa hii rasilimali ya Nishati Jadidifu ili wananchi wetu wajue jinsi serikali yao ilivyojipanga kuendeleza nishati hizo,” amesema Nyanda na kuongeza kuwa:

“Changamoto nyingine iliyokuwepo ni Sera ya Mkakati wa Nishati Jadidifu na jinsi gani unapata nyenzo ya kutekeleza sera yako inayotambua nishati Jadidifu ndio maana sasa hivi serikali imewekeza katika kuandaa Mkakati ya Nishati Jadidifu na Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati,” amesema Nyanda.

Hata hivyo Nyanda ameongeza kuwa mbali na mkakati huo pia wanaandaa mkakati wa matumizi bora ya nishati ili viende pamoja na sera ya mkakati wa nishati jadidifu.

Baadhi ya Waandishi wa habari walioshiriki katika mafunzo ya nishati jadidifu.

Kwa upande wake Mratibu wa Mabadiliko ya Tabianchi na Tungamotaka kutoka TaTEDO, Shima Sago amesema wanazungumzia Nishati Jadidifu hasa wakati huu kutokana na kwamba nishati zingine zinachangia uharibifu wa tabaka la juu linazozuia mionzi ya jua kufika ardhini hivyo kusababisha ongezeko la joto na ukame.

“Faida za Nishati Jadidifu ni pamoja na kupunguza gharama za kununua umeme mara kwa mara,kutoa ajira,kukaushia vyakula shambani,kuepuka matatizo ya kiafya kwa kuvuta hewa chafu,kupunguza hewa ukaa na kutunza tabaka la kuzuia mionzi ya jua.

“Ili upate tani moja ya mkaa lazima ukate magogo 12 ya miti na kwa mwaka tunatumia tani Milioni 2.5 za mkaa nchini hivyo ni lazima tuendeleze kuhifadhi mazingira na kutumia nishati jadidifu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,”amesema Sago.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles