28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI INAWEZA KUONGEZA MAPATO  KWA KUKUSANYA KODI

 

Na FREDRICK KATULANDA-DODOMA


TANGU kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, kumekuwa na jitihada mbalimbali za kukabiliana na wabadhirifu wa mapato ya Serikali pamoja na kuhakikisha mapato ya kodi yanakusanywa kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa kodi na utoroshwaji wa mali na fedha nje ya nchi.

Jitihada hizo zimekuwa zikiendelea kushika kasi na kutekelezwa, ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akiwa na dhamana ya kusimamia jukumu hilo alisema iwapo Serikali itafanikiwa kusimamia vyema ukusanyaji kodi, Taifa linaweza kuepukana na aibu kwa viongozi wake kwenda nje ya nchi kuomba misaada.

Jitihada za kukusanya mapato zilizoanzishwa chini ya Rais Magufuli zimekuwa chachu ya TRA kuvuka lengo kwa kukusanya kodi Sh trilioni 1.4 Desemba 2015, lakini bado inaelezwa kuwa kodi zaidi inaweza kukusanywa.

 

Katika kuhakikisha lengo la Serikali linafikiwa la kuongezeka kwa mapato, wadau wa Mtandao wa Haki ya Kodi Tanzania (Tanzania Tax Justice Coalition – TTJC), walifanya utafiti wao na kutoa mapendekezo ya kufanyiwa kazi na Serikali ili kusaidia kuboresha ukusanyaji na matumizi ya mapato ya fedha za umma.

Katika taarifa ya TTJC iliyowasilishwa kwenye kongamano la wadau ndani na nje ya Tanzania, lililolenga kujadili, kujifunza na kushirikishana uzoefu katika utetezi na usimamiaji wa michakato ya maamuzi ya rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia viwe chachu ya maendeleo kwa Taifa, andiko lililojulikana kama TEIC 2017.

Taarifa ya utafiti wa TTJC ilibainisha kuwa Serikali kwa umma inahitaji rasilimali mbalimbali, zikiwemo fedha na kwamba kushindwa kwake kukusanya mapato ya kutosha kunadhoofisha utoaji wa huduma bora kwa Watanzania.

Walisema tafiti mbalimbali zinaonesha Tanzania inapoteza kiwango kikubwa cha mapato yanayotokana na kodi na kubainisha mwaka 2012, Kamati ya Viongozi wa Dini ya Masuala ya Haki za Kiuchumi na Uadilifu katika Uumbaji walitoa ripoti iliyothibitisha hayo.

Walieleza ripoti ya viongozi wa dini ilibainisha kiwango cha upotevu wa mapato kilikuwa ni Dola kati ya milioni 847 na bilioni 1.3, ikiwa ni upotevu wam apato kwa njia mbalimbali ikiwemo misamaha ya kodi na utoroshwaji fedha kwenda nje ya nchi.

Hali ya sasa bado tete kwani inaonesha upotevu wa kodi umeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.83, sawa na fedha za Kitanzania takribani Sh trilioni 4.

Washiriki walielezwa fedha hizo zilizopotea zingeweza kufadhili mara tatu bajeti ya Sekta ya Afya au mara mbili bajeti Sekta ya Elimu kwa mwaka 2016/17.

Walisema licha ya utafiti uliofanyika mwaka 2017 kuonesha kuongezeka kwa jitihada katika kukusanya mapato, bado Serikali inakabiliwa na matatizo kama ya ukwepaji wa kodi, upotevu mapato kwenye misamaha ya kodi, utoroshwaji wa mali na fedha nje ya nchi na upotevu mwingine katika manunuzi ya umma.

TTJC ni nini?

Kama anavyoeleza Meneja wa Uchambuzi wa Sera kutoka mtandao wa Policy Forum Nicholas Lekule, taasisi hii ya Wadau wa Haki ya Kodi Tanzania ilianzishwa mwaka 2015 chini ya uratibu wa asasi ya Policy Forum ikiwaunganisha wadau mbalimbali kutoka asasi za kiraia pamoja na watu binafsi ambao wana kiu ya kuona haki katika kodi inapatikana nchini.

Alisema malengo ya taasisi hiyo ni kujikita katika tafiti mbalimbali ambazo zina lengo la kuhakikisha mianya yote ya upotevu wa fedha za umma inajulikana na inazibwa.

Kufanya uchambuzi wa nani anayelipa kodi na kiasi gani ili kuhakikisha kila mtu au taasisi inalipa kodi stahiki na kukemea vitendo vyote vinavyohusiana na ukwepaji kodi.

Tangu kuanzishwa kwake, taasisi hii imefanikiwa kufanya chambuzi mbalimbali kwenye miswada ya sheria kadhaa ikiwemo mswada wa sheria ya usimamizi wa kodi, mswada wa sheria ya kodi ya ongezeko la thamani.

Taasisi  imekutana na kujadiliana na watengeneza sera wakiwemo wabunge, viongozi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, TRA kwa lengo la kushirikishana matokeo ya tafiti zake na kupendekeza namna Serikali inavyoweza kuboresha hatua za ukusanyaji wa mapato yake.

Kuhusu misamaha ya kodi:

Anasema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/16, inaonesha Serikali ilitoa misamaha ya kodi ya Sh trilioni 1.10 sawa na asilimia 1.14 ya pato la ndani la taifa, wakati lengo ni kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia chini ya asilimia moja ya pato la ndani.

CAG alibaini misamaha ya kodi imekuwa ikitumika kuwanufaisha watu au makampuni yasiyostahili. Mfano kwa kipindi cha mwaka 2012 hadi 2014, magari 238 kutoka nje ya nchi yaliingizwa nchini kwa kutumia majina ya walipa kodi wawili ambao hawakustahili na mwaka 2015/16 Serikali ilipoteza Sh billioni 3.46 kwa kutoa misamaha ya kodi kwa watu wasiostahili.

Akizungumzia kuhusu utoroshwaji wa fedha na manunuzi, alisema viwango vipya vya upotevu wa mapato kwa utoroshwaji wa fedha nchini vinaonyesha kwa sasa ni Dola milioni 464 kwa mwaka.

CAG pia katika manunuzi ya umma 2015/16, alibaini mapungufu katika utaratibu wa utoaji wa zabuni, utekelezaji na usimamizi wa mikataba na manunuzi ambayo hayakufanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni. Imebainika kwamba watu wachache sana tena walio kwenye sekta rasmi ndio wanaolipa kodi na hivyo kubeba mzigo wote wa wale wasiolipa kodi.

Ripoti ya CAG 2015/16 inaonesha takriban Sh 588.8 bilioni hazikukusanywa kutoka kwa walipa kodi mbalimbali.

Uchunguzi uliofanyika mwaka 2015 hadi 2016 ulibaini katika walipakodi 9,743 waliosajiliwa kukusanya kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ni walipa kodi 1,578 ambao ni asilimia 16 tu ndio wanatumia mashine za EFD. Kati ya walipakodi 49,009 wanaostahili kutumia mashine za EFD ni walipakodi 9,127, ambao ni asilimia 18.6 tu wenye mashine hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles