Na CLARA MATIMO-MWANZA
KILIO cha muda mrefu cha wanawake wajasiriamali wa Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza kukosa kiwanda cha kisasa cha kuchakata maziwa kimepata mwarobaini baada ya kuanza ujenzi wa kiwanda hicho.
Kiwanda hicho kinachokithi viwango vya kisasa vya matakwa ya Serikali kinajengwa katika Kata ya Kahumulo wilayani humo na Shirika lisilo la Serikali la Mikono Yetu linalojishughulisha na kuwawezesha wanawake na wasichana kumiliki rasilimali zalishi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (Sido) Mkoa wa Mwanza, Bakari Songwe, akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa katika Kijiji na Kata ya Kuhumulo, alisema wilaya hiyo inavyoviwanda ambavyo vinachakata mazoa mbalimbali ya chakula lakini haikuwa na kiwanda kinachochakata maziwa.
Alisema kutokuwa na kiwanda kama hicho, kulisababisha wanawake wengi wa maeneo hayo kukosa fursa mbalimbali za kujiongezea kipato kupitia mazao ya mifugo wanayoifuga hasa ng’ombe.
“ Wanawake wengi kati yenu ambao mlipata mafunzo kutoka sido mmekuwa mkitwambia mnatamani muwe na kiwanda cha kuchakata maziwa, Shirika la Mikono Yetu limesikia kilio chenu wito wangu msikumbatie ujuzi mlio nao mshirikishane ili muweze kutengeneza vitu vyenye ubora na ushindani,”alisema Songwe.
Meneja Programu wa Shirika la Mikono Yetu, Sophia Nshushi, alisema ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu Sh milioni 30 lakini hadi sasa wana Sh milioni 15 ambazo wamezipata kutoka Womenfirst International Fund nchini Marekani, Shirika lisilo la Serikali linalotetea haki za wanawake (Kivulini) lenye makao yake jijini Mwanza na wanawake wenyewe wanashiriki kwa kuchota maji na kufanya kazi wanazoziweza.
“Kiwanda hiki kikikamilika kitawanufaisha wanawake zaidi ya 150 kwa sababu hadi sasa bado wengine wanazidi kujiunga kwenye vikundi ambao wamekwishajiunga ni zaidi ya 110, lengo la Mikono Yetu ni kukuza biashara za akina mama kwa kuzirasimisha, nawaomba wahisani mbalimbali watakaoguswa watuunge mkono ili kikamilike mapema.
“Tumeamua kuwajengea wanawake wa Kahumulo kiwanda kwa sababu asilimia kubwa ya watanzania wanaishi vijijini na vijijini wengi ni wanawake, kiwanda hiki kikikamilika kitakuwa kinazalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao pamoja na mifugo ambavyo vinapatikana maeneo haya,”alisema.