ZANZIBAR iko katika hatua za mwisho za utengenezaji wa Sera ya Viwanda ili kuwezesha ukuaji wa Sekta hiyo kufuatia mahitaji yake ambayo kukosekana kwake kumesababisha ukuaji mdogo wa uwekezaji ukifananisha na kile kinachofanyika bara ambako kumeshamiri.
Sera ya viwanda mara nyingi hutambua mahitaji halisi ya nchi husika na kuweka vigezo stahiki vya uwekezaji vikiambatana na utoaji mwafaka wa vivutio kwa kwa wawekezaji wanaounga mkono sera hiyo kama ilivyoainishwa.
Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ya Zanzibar imesema sekta ya viwanda inazidi kuimarika katika thamani ya uzalishaji viwandani kutoka Shilingi bilioni 4.17 hadi kufikia Shilingi bilioni 4.87 kwa mwaka jana ikiwa ni ukuaji wa asilimia 12.
Balozi Amina Salum Ali ambaye ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko alisema hayo wakati akitoa maelezo mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Unguja na kubainisha hatua waliyofikia kwa kuelezea hatua iliyofikiwa ya sera ya Viwanda na kutoa umuhimu wake kwa sekta binafsi na kuipongeza kwa mchango wake chanya.
“Tupo katika hatua za mwisho za mchakato wa kukamilisha sera ya viwanda itakayokuwa mwongozo katika kuimarisha sekta hiyo na kuchangia pato la taifa…, lakini tunaipongeza sekta binafsi kwa kuitikia wito wa uwekezaji wa viwanda,” alisema Balozi Amina.
Kabla ya maelezo hayo Dk Shein alifurahishwa na mazingira yaliyooneshwa ya wawekezaji kuchangamkia kuwekeza katika sekta za viwanda huku akisisitiza kwamba Serikali yake imeimarisha mazingira ya uwekezaji na ikikamilika sera itakuwa kivutio kwa wawekezaji wengi
Alizitaka taasisi za uwekezaji Zanzibar ikiwemo Mamlaka ya Vitega Uchumi (ZIPA) kujenga mazingira mazuri yatakayowafanya wawekezaji kuja kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ripoti zilizopo zinaonesha kuwa uwekezaji huo umeimarika zaidi katika viwanda vya kazi za ujenzi ikiwemo kusaga kokoto pamoja na matofali.
Waziri huo alisema uwekezaji katika Kampuni ya Azam umeongeza uzalishaji wa bidhaa za maziwa na hivyo kuongeza ajira.
Alivitaja viwanda vingine vilivyoimarisha uzalishaji na ajira kuwa ni pamoja ni viwanda vya maji ya chupa.
Wakati huo huo habari toka Pemba zinaonesha kuwa shughuli ya kutafuta mafuta imeanza visiwani humo.
Utafutaji mafuta
Kazi za utafiti wa nishati ya mafuta kwa kutumia meli zinatarajiwa kuanza katika ukanda wa Kisiwa cha Pemba kwa mujibu wa taarifa ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi amabaye amezindua utafutaji wa nishati ya mafuta kwa kutumia meli baharini leo.
Mtaalamu wa mafuta kutoka Kampuni ya Rakgas ya Rasilkhema, Sharif Hassan alisema kazi za utafiti zitafanywa na Kampuni ya BGP kutoka China kwa kutumia meli katika ukanda wa bahari ya Pemba na Unguja.
Akifafanua, alisema kazi za utafiti wa mafuta kwa njia ya bahari zimezingatia athari zote za mazingira ikiwemo kwa wavuvi na viumbe vya baharini ili wasipate matatizo yanayoweza kuzuilika
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira, Ali Halil Mirza alisema hatua iliyofikiwa sasa ni kufanya utafiti kujua kama nishati ya mafuta ipo au hakuna.
“Tumezingatia masuala ya athari za mazingira kwa viumbe wa baharini ambapo kabla ya kufanya kazi hiyo, utafiti zaidi utafanyika kujua aina ya samaki waliopo baharini na rasilimali nyinginezo zitakazoweza kuvunwa kikamilifu, ” alisema Hassan wa BGP.
Mirza alisema utafiti uliofanyika katika hatua za kwanza ulikuwa wa kupigapicha ardhini kwa kutumia ndege ambayo matokeo yake yanafanyiwa uchambuzi na yanatazamiwa kujulikana kwa ukamilifu wake hivi karibuni.
Hassan alibainisha kuwa kazi zinazofanyika kwa sasa ni utafiti wa mafuta uliofanyika kwa njia ya kupiga picha kwa kutumia ndege ardhini .