Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Serikali imeeleza kuwa sekta ya kilimo nchini inatarajia kuzalisha ajira milioni 30 ifikapo mwaka 2030 hatua mbayo itachochewa na nyanja hiyo kufikia asilimia 10 ya mchango wake katika pato la Taifa.
Hayo yamebainishwa Mei 23 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dk. Hussein Omar wakati wa kikao kazi cha makubaliano ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata mbolea na kampuni ya OCP Ltd ya Morocco kwa kushirikiana na TFC ambapo amesema lengo la uwepo wa viwanda hivyo nchini ni kurahisisha upatikanaji wa mbolea ambayo itauzwa Kwa bei ambayo itamnufaisha mkulima.
“Pamoja na uwepo wa viwanda hivyo ipo fursa ya kuchakata takataka na kuzifanya kuwa mbolea hali itakayosaidia pia kuongeza ajira na kusafisha majiji.
“Hadi kufikia mwaka 2023 kupitia kilimo, ajira millioni 3 zimetolewe na takataka ambazo zimekuwa kero kwenye majiji yetu zimechakatwa na kuwa mbolea. matarajio yetu ni kwamba kufikia mwaka 2030 sekta hii ya kilimo itakuwa imezalisha ajira milioni 30,” amesema.
Nae Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Samuel Mshote amesema wamefikia makubaliona ya ujenzi wa viwanda vya mbolea pamoja na usambazaji wa mbolea iliyozalishwa na kampuni ya OCP ambayo imeshaingizwa nchini ili kuwasaidia wakulima.
“Mbolea itakayosambazwa ni Ile ya kupandia kukuzia pamoja na virutubishi ambapo tani laki Moja zimeshaingia nchini,”amesema Mshote.
Amesema lengo ni kuona mbolea inamfikia mkulima kwa wakati na kwa bei nzuri hivyo watahakikisha inawafikia wakulima wote nchini.
Aidha, Mshote amasema ili kuwafikia wakulima wote kutakua na kituo cha pamoja katika mikoa na kutafanyika mafunzo kwa wakulima namna bora ya kutumia mbolea hiyo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa kampuni ya OCP Afrika, Youssef Lahmiti amesema mchakato wa ujenzi huo utaanza mapema na watatoa elimu ya uchakataji wa mbolea za takataka kwa muda mfupi badala ya mfumo uliozoeleka unaotumia siku 100 badala yake utatumia siku 3 tu.