26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii yahimizwa kutoa fursa sawa kwa watoto ili kutokomeza ukatili wa kijinsia

*KOICA yapiga tafu vifaa vya kusaidia Uwezeshaji Wanawake Singida, Shinyanga

Na Mwandishi Wetu,Mtanzania Digital

Ili jamii ifikie usawa wa kjiinsia ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha watoto wanapewa fursa sawa katika nyanja zote ambazo ni elimu, ushiriki katika shughuli za kiuchumi, kimaamuzi na kupinga kwa nguvu zote vitendo vya unyanyasaji na ukatili ambavyo vinatweza jinsia ya kike.

Wito huo umetolewa leo Mei 24, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mboni Mhita kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Christina Mdeme, katika hafla ya makabidhiano ya Mradi wa kufikia usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake na wasichana balehe kwa kuwainua kiuchumi wilayani Msalala mkoani Shinyanga.

Mhita amesema kuwa kuendelea kuwapo kwa vitendo vya ukatli wa kijinsia kunachochea kuendelea kuwapo kwa mimba na ndoa za utotoni.

“Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kwamba watoto wanapewa fursa sawa katika nyanja zote ambazo ni elimu, ushiriki katika shughuli za kiuchumi, kimaamuzi na kupinga kwa nguvu zote vitendo vya unyanyasaji na ukatili ambavyo vinatweza jinsia ya kike.

“Jambo hili linasababisha kuongezeka kwa mimba na ndoa za utotoni ikiwamo pia kuongezeka kwa watoto waishio katika mazingira hatarishi na kaya zinazoishi katika hali ya umasikini,” amesema Mhita.

Akizungumzia mradi huo, Mhita amesema kuwa umechochea mabadiliko chanya juu ya kuhakikisha mila zinazowanyima wanawake na mabinti fursa za ushiriki wao katika maeneo ya kiuchumi, elimu, afya na katika kushangia kipato cha kaya zinaachwa nyuma kwani zilikuwa zikiwachelewesha.

“Kupitia mradi huu wanawake wamekuwa wakishriki katika fursa za kilimo cha uzalishaji ikiwamo matunda na mbogamboga na kujipatia kipato kinachowezesha familia zao kuendelea kustawi.

“Mbali na hilo, mabanti 450 wamepata fursa ya mafunzo ya ufundi ambapo wamekuwa majasiri katika kuukabili unyonge wao ndani ya jamii ambao awali ulionekana kuwa kumwezesha mtoto wa kike ni kupoteza fedha,” amesema Mhita.

Mradi huo unahusisha vituo vitano vipya vya kusaidia uwezeshaji wa wanawake na kukabiliana na ukatili wa kijinsia ambavyo vimekabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania katika Mikoa ya Singida na Shinyanga, kupitia msaada wa UNFPA na UN Women, unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa (KOICA).

Katika vituo hivyo vitano, vitatu ni vya One Stop Centre, Dawati moja la Jinsia na Watoto la Polisi, na Kituo kimoja cha Makusanyo, na mafunzo na programu zinazohusiana, tayari vimeongezwauwezo kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia (GBV) na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

Ikumbukwe kuwa hatua hiyo ni moja ya mafanikio ya Mpango wa Pamoja wa Kutambua Usawa wa Kijinsia kwa Kuwawezesha Wanawake na Wasichana Vijana ambao sasa uko katika mwaka wake wa mwisho (2020-2023) ulifadhiliwa na KOICA kwa dola milioni 4.9.

Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini Tanzania, Shin Manshik.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini Tanzania, Shin Manshik, kupitia mpango huo zaidi ya watu 10,000 wamefikiwa ili kuongeza ujuzi wa haki zao, kusaidia usawa wa kijinsia, na kupanua uwezo wa kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia, na kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika Mikoa ya Singida na Shinyanga.

“Tunapongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi.

“KOICA inatarajia kutoa huduma muhimu za kisheria, kijamii na kimatibabu kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia kupitia Vituo vya Pamoja ambavyo vilijengwa na Mradi wetu,” amesema Manshik, na kuongeza kuwa:

“Pia, tunatarajia kuona uwezeshaji na ukuaji thabiti wa vikundi vya wanawake vya kilimo ambavyo vitachangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania katika siku zijazo kwa kusaidia Kituo cha Ukusanyaji,” amesema.

Kituo cha One Stop Centre katika Kituo cha Afya cha Bugarama mkoani Shinyanga tayari kinafanya kazi; Vituo vya One Stop Centres vya Hospitali ya Wilaya ya Ikungi na Hospitali ya Rufaa ya Singida mkoani Singida vimefunguliwa.

Melissa McNeil-Barrett, Naibu Mwakilishi wa UNFPA akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Kwa mujibu wa Melissa McNeil-Barrett, Naibu Mwakilishi wa UNFPA, vituo hivyo, kwa kuzingatia misingi ya vituo vya afya, vinakuza mtazamo unaozingatia waathirika wa ukatili dhidi ya wanawake katika mazingira ya kuunga mkono, na kuwapa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia msaada wa kiafya, kisheria, na kisaikolojia wote chini ya paa moja.

“Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi Bugarama, ambalo sasa limezinduliwa rasmi, linawapa wale walio katika hatari ya ukatili na watu walio katika hatari ya usaidizi wa kisheria wa heshima na siri na huduma za rufaa kwa vituo vinavyofaa. Vituo vya Pamoja na Madawati ya Jinsia na Watoto ya Polisi, vyote katika majengo mapya yaliyojengwa, vinaboresha miundombinu na kuimarisha uwezo wa ndani ili kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijisnia na vitendo vyenye madhara.

“Uanzishwaji wa vituo hivi vya One Stop Centre, na Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi vinawakilisha hatua kubwa katika kuimarisha taasisi za ndani ili kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia,” alisema Melissa na kuongeza kuwa:

“Athari chanya za programu hii ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya kesi za ukatili wa kijinsi zinazoripotiwa na kupelekwa,” amesema.

Upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake nchini Tanzania (UN Women), Hodan Addou, amesema kituo cha Makusanyo kilichopo Wilaya ya Ikungi, Mkoa wa Singida nacho tayari kinafanya kazi na kwamba hiyo inawezesha idadi kubwa ya wanawake na vijana wanawake wakulima wadogo wadogo wanaouza mazao ya bustani kukusanya na kuhifadhi mazao yao, na hivyo kuimarisha masoko ya pamoja, kuboresha utunzaji baada ya kuvuna, na kuinua uchumi.

“Uwezeshaji wa kiuchumi ni njia muhimu ya kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

“Juhudi za Mpango wa Pamoja, ikiwa ni pamoja na: Kituo cha Pamoja, haki za umiliki wa ardhi zinazozingatia jinsia, na pembejeo kwa ajili ya uzalishaji wa kilimo, zote zinasaidia wanawake kuboresha kipato na uwezo wao wa kustahimili kwa kipimo.

“Kwa ushirikiano na mamlaka za mitaa, tunajivunia kusaidia mamia ya wakulima wanawake na vijana wa kike kufurahia haki zao, kujenga uwezo wao, na kupanua uwezo wao wa kiuchumi,” alisema Addou.

Aidha, Addou ameyataja mafanikio ya jumla ya mpango huo kiuwa ni kutoa mafunzo kwa wafanyakazi zaidi ya 450 (kwa wafanyakazi wa afya, wasaidizi wa kisheria, maafisa wa polisi) juu ya kuzuia na kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi katika vituo vya One Stop Centres. Takriban wafanyakazi 300 wa huduma za afya wamepewa mafunzo ya usimamizi wa kesi za ukatili wa kijinsia, wakiwemo wafanyakazi kutoka vituo vya One Stop Centre.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles