KUNDI la muziki wa asili la Segere Original, limesema kwamba limeachana na matamasha ya hotelini kwa kuwa hayawalipi kama ilivyokuwa zamani.
Mkurugenzi wa kundi hilo, Karama Tolly, alisema zamani walikuwa wakitegemea matamasha hayo maalumu na hoteli zilizokuwa zikiwalipa vizuri lakini wameachana na muziki wa kupiga hotelini kwa kuwa hazilipi vizuri.
“Awali tulikuwa tukipiga muziki katika hoteli mbalimbali zilikuwa zikilipa vizuri lakini kutokana na mabadiliko ya muziki na ugumu wa uchumi tumeamua kuachana na kazi hizo kwa kuwa wanalipa Sh 120,000 kwa onyesho kiasi ambacho akikidhi mahitaji yetu.
“Kwa fedha hiyo tunawezaje kubeba vyombo kupeleka hoteli, kulipa wasanii wa kundi na kujilipa ndiyo maana kwa sasa tumeamua tutegemee shoo za matukio maalumu yakiwemo ya kitaifa na kimataifa badala ya shoo za hotelini,” alieleza Tolly.
Katika hatua nyingine, Karama alisema kwa sasa wanatafuta mdhamini kwa ajili ya kufanya video ya wimbo wao mpya wa ‘Shangazi’ wanaotarajia kuuachia mara baada ya video hiyo.
“Muziki huo tumeimba mfumo wetu wa Segere lakini tumeongeza na singeli kidogo ili kuongeza ladha katika muziki wetu wa asili. Ila tunaamini video hiyo ikikamilika itaturudisha tulikokuwa na kutuongezea kujulikana zaidi kwa kuwa tumekuja kivingine,” alisema.