24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SAUTI YA LISSU YAMUIBUA RIDHIWANI KIKWETE

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


SIKU moja baada ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kuzungumza kwa mara ya kwanza tangu alipopigwa risasi   Dodoma, wabunge na wananchi mbalimbali wamezidi kumuombea apone haraka.

Mmoja ya wabunge wa CCM ambao walimtaka heri Lissu ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), ambaye amesema   amefurahia kumuona   kiongozi na mwanakamati mwenzake.

“Mungu hutenda wema siku zote. Ashukuriwe yeye kwa kazi ya kurejesha tabasamu katika sura yako na afya kwa wanaokuuguza. Nimefurahi kukuona tena msomi, kiongozi wangu na mwana kamati mwenzangu wa Bunge ukitabasamu na mwenye afya njema.

“Mungu akulinde na akusimamie katika matibabu yako. Looking forward to see you back into your good shape. #prayfortundulissu,” aliandika Ridhiwani katika akaunti yake ya mtandao wa  jamii wa Facebook

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema   amefarijika kusikia tena sauti ya Lissu ambayo imeboreka zaidi.

Alisema Watanzania wamefarijika kusikia na kuona bado kiongozi huyo yuko hai na ataweza kuungana nao tena kuendeleza mapambano ya kujenga demokrasia.

“Jana (juzi),  nimefarijika kukusikia tena sauti yako tangu nikusikie nilipokuja kukusabahi hospitalini. Sauti yako sasa imeboreka na kurudi sauti ile ile uliyokuwa nayo kabla hujashambuliwa kwa risasi nyumbani kwako Dodoma.

“Watanzania wamefarijika sana kuwa bado uko hai na utaweza kuungana nasi tena kuendeleza mapambano ya kujenga domokrasia yetu.

“Siku ile nimekuja kukusabahi uliniuliza nini kinaendelea nyumbani. Nilikwambia tu Watanzania wanakuombea. Ukanitazama kwa lile jicho lako la kiMarx, ukacheka na kusema “Taifa la Waomba Mung. Tukacheka”.

“Ni kweli Watanzania wamekuombea sana na ni jambo la kushukuru kuwa Mola amewasikiliza maombi yao. Hata hivyo, kuna mengi yanaendelea nchini kwetu. Uchumi wa Taifa sasa umeshuka mno kiwango cha kutilia shaka hata takwimu rasmi za Serikali,” alisema Zitto katika barua yale kwenda kwa Lissu.

Zitto alisema   wakulima wana vilio nchi nzima hasa katika mazao ya mbaazi, korosho tumbaku na kote hali si nzuri.

“Yote hayo yakiendelea, CCM inafanya juhudi kubwa kuhamisha mjadala kuhusu waliokushambulia kwa kununua madiwani na wanachama wa vyama vya upinzani kila siku, wakiubana zaidi uhuru wa habari na wakiuzima uhuru wa vyama vya siasa.

“Hawataki kabisa mawazo mbadala ya kututoa katika hali tuliyonayo. Utakaporudi naamini utakuta mengine mengi mapya.

“Ninafuraha kuwa unaendelea vizuri sana tofauti na nilipokuja kukuona . Tutazidi kumwomba Mola afya yako iimarike zaidi.

“Tuna kazi kubwa sana mbele ya safari na kwa hakika ni lazima tuifanye kwani tusipoifanya nchi yetu itaanguka uchumi na demokrasia na watu wetu kuendelea kuwa masikini,” alisema Zitto.

Alisema lengo la waliomshambuliwa Lissu ni kuwanyamazisha ingawa wamewaambia kuwa hatutanyamaza kamwe.
“Kama ulivyoniambia ukiwa kitandani kuwa “Tumeshashinda,  Tutashinda”. Hakika ushindi ni dhahiri na ndiyo maana wanatapatapa kuzuia uhuru wa mawazo na fikra.

“Ndugu yangu, nisikuchoshe na barua ndefu kwani najua bado hujawa na nguvu za kutosha. Nilikuletea kitabu nikamwambia mkeo awe anakusomea.

“Naamini anafanya hivyo. Juzi tulisherehekea miaka 50 tangu kuuawa kwa komredi Che Guevara. Najua unavyompenda Che tungekutana ubalozi wa Cuba hapa Dar siku ile,” alisema katika barua hiyo kwenda kwa Lissu.

Kwa mara ya kwanza tangu ajeruhiwe kwa risasi Septemba 7, mwaka huu, sauti ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ilisikika juzi.

Lissu ambaye amelazwa katika Hospitali ya Nairobi alitumia dakika tatu kutoa shukrani zake kwa Mungu kwa kusikia maombi ya waja wake na hivyo kutimiza siku 42 hadi sasa akiwa hai.

Pia Lissu aliwashukuru watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ambao wamejitoa kwa hali na mali katika kumsaidia wakiwamo madaktari na wauguzi.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika  (TLS), alisema kama si mkono wa Mungu uhai wake ulikuwa umekatishwa nyumbani kwake Dodoma.

“Watanzania wenzangu mimi ni Tundu Lissu, nazungumza kutoka kitanda cha Hospitali ya Nairobi. Kwanza kabisa naomba nitoe shukrani zangu kwa Mungu wetu kwa mapenzi, Mungu  wetu wa maisha, Mungu wetu wa uponyaji kwa kuniweka hai mpaka hapa nilipo.

“Kama isingekuwa Mwenyezi Mungu, maisha yangu yangeishia nyumbani kwangu Dodoma siku ile. Lakini Mwenyezi Mungu huyu wa uponyaji, Mwenyezi Mungu alisema huyu hatakufa, naomba nishukuru kwa hilo kwanza.

“Pili Watanzania kwa mamilioni yao kila mahali walipo, walioko Tanzania, walioko nchi za nje, walioko mataifa mbalimbali duniani nao vilevile walipaza sauti makanisani, kwenye mikutano ya hadhara, misikitini, na kumwomba Mungu maisha yangu yapone.

“Nafikiri sitakosea nikisema kwamba niko hai kwa sababu ya maombi ya mamilioni ya Watanzania hawa vilevile,” alisema Lissu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles