29.1 C
Dar es Salaam
Sunday, December 15, 2024

Contact us: [email protected]

‘Sauti ya Jamii kiwe chachu kwa vikundi vingine’

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, amekipongeza Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni kwa kuwa mfano mzuri katika kutekeleza sera za wizara hiyo.

Mwonekano wa jengo la kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni.

Dk. Gwajima ametoa pongezi hizo wakati akizindua jengo la kikundi hicho ambacho kinajishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kukemea vitendo vya kikatili.

Amesema baada ya kukitembelea Machi nane mwaka huu wakati wa kutoa tamko la siku ya wanawake duniani alivutiwa na shughuli mbalimbali wanazozifanya ambazo ni nadra kuzikuta sehemu nyingine.

“Nimefarijika sana kuja Kipunguni kwa sababu ni eneo linalonifanya nipate mfano mzuri jinsi gani jamii ya Kipunguni imejipanga kutekeleza sera za wizara zinazohusu maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu.

“Sio rahisi kusimamisha mfumo ukawa wa mfano, mimi nazunguka kila mtaa najua, nyie (Kipunguni) ni wa mfano… nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya, tutaendelea kuwaangalia ili kadiri mnavyoendelea kufanya vizuri tupate cha kusema kaige pale.

“Nina imani siku nyingine tukija tutakuta ofisi kubwa zaidi kwa sababu mtaendelea kukua na mtalea vikundi vingine vinavyochipuka ili kasi ya maendeleo ikaenee na kuambukizana kutoka kikundi kimoja kwenda kingine,” amesema Dk. Gwajima.

Amesema kikundi hicho kimeleta tija kwa wananchi wa Mtaa wa Amani, Kata ya Kipunguni na halmashauri kwa ujumla na kukitaka kikawe chachu kwa vikundi vingine nchini.

“Tuna vikundi vingi lakini pamoja na kazi njema tunayofanya lazima sasa tuombe maeneo, tununue na halmashauri zote ziwaangalie kama ni wadau ili wahakikishe kwamba mnakuwa na mahala pa kuweza kukutana na kufanya kazi zenu.

“Hatutarajii vikundi vife, tunatarajia viendelee miaka mingine mingi virithishe kwenye jamii inayokuja,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa kikundi hicho, Seleman Bishagazi, amesema jengo hilo lililogharimu Sh milioni 11.9 limejengwa kwa fedha zao wenyewe.

Amesema jengo hilo lina vyumba viwili yaani ofisi na chumba cha kutolea mafunzo ya ushonaji na mengine ya ujasiriamali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kipunguni, Steven Mushi, amesema wanaendelea kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ambapo kwa mwaka 2020/21 walitoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 587 iliyovinufaisha zaidi ya vikundi 50.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles