32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SARATANI ILIPOTOKA, INAVYOENEA NA SIFA ZAKE

uvutaji-wa-sigara-unaweza-kusababisha-saratani-ya-mapafu
Uvutaji wa sigara unaweza kusababisha saratani ya mapafu

 

Na JOACHIM MABULA,


 

SARATANI ni kundi la magonjwa yanayosababishwa na mgawanyiko usio sawa na usiodhibitika wa seli na kuunda uvimbe unaovamia na kuzidhuru tishu. Saratani isiyotibiwa inaweza kuwa ugonjwa unaoshambulia tishu nyingine mwilini na kusababisha kifo. Saratani huusababishia mwili madhara pale inapoharibu seli na kuzifanya zigawanyike bila kudhibitika na kuwa uvimbe wa tishu unaojulikana kama tumor, isipokuwa katika saratani ya damu ambapo huzuia utendaji wa kawaida wa damu kwa kuzifanya seli ziwe na mgawanyiko usio wa kawaida.

Imetoka wapi?

Asili ya neno kansa linatokana na daktari bingwa wa Ugiriki aliyeishi kati ya miaka 460 na 370 K.K aitwaye Hippocrates. Hippocrates alitumia maneno ‘Carcinos’ & ‘Carcinoma’ kuelezea uvimbe unaotengeneza mchubuko na uvimbe usiotengeneza mchubuko. Maneno haya ya Kigiriki yana maana ya mdudu kaa. Ugonjwa ulifananishwa na kaa kwa kuwa unasambaa kila upande kama miguu ya mdudu kaa. Kati ya miaka 25 na 50 K.K, daktari bingwa mroma aitwaye Celsus alitafsiri maneno hayo kwa neno la kilatini ‘Cancer’ lenye maana ya mdudu kaa. Miaka kati ya 130 na 200 B.K daktari bingwa mwingine kutoka Ugiriki alitumia neno ‘Oncos’ lenye maana ya kuvimba kuelezea vimbe tofauti zisizosambaa. Hata hivyo, maneno ya Hippocrates & Celsus ‘Carcinos’ & ‘Cancer’ yenye maana ya mdudu kaa ambayo bado hutumika kuelezea vimbe zinazosambaa. Neno la Galen ‘Oncos’ linatumika tu kama sehemu ya somo linalohusu kansa ‘Oncology’au madaktari wa saratani ‘Oncologist’.

Chanzo chake

Mwili wa binadamu umeundwa kwa trilioni za seli ambazo hukua, kugawanyika na kufa kwa mpangilio maalumu. Mwenendo ulioratibiwa vyema unasimamiwa na vinasaba (DNA) vilivyo ndani ya seli. Vinasaba(DNA) vinapatikana katika kila seli na huongoza matendo yote yanayofanywa na seli. Katika seli ya kawaida wakati vinasaba vinapoharibika seli hukarabati au seli hufa. Lakini katika seli za saratani, kinasaba kilichoharibika huwa hakiwezi kukarabatiwa na seli haifi kama inavyotakiwa badala yake huendelea kutengeneza seli nyingine ambazo hazitakiwi na mwili na seli hizo mpya zote huwa na kinasaba kisichokuwa cha kawaida tofauti na seli salama.

Watu huweza kurithi kinasaba kisichokuwa cha kawaida lakini mara nyingi uharibifu wake husababishwa na makosa yanayotokea wakati seli ya kawaida inapotengenezwa au kutokana na sababu za kimazingira. Ingawa inajulikana wazi kuwa kuna baadhi ya vitu vinavyoweza kuharibu kinasaba na kusababisha saratani kama vile kemikali, uvutaji sigara, kuchomwa na jua na kadhalika lakini bado hakuna uhakika wa moja kwa moja kuhusiana na kinachosababisha saratani.

Wakati mtu anapokuwa mtoto mdogo au bado akiwa ndani ya tumbo la mama, seli hujigawanya kwa haraka ili kumfanya akue. Baada ya mtu kukua, seli nyingi hugawanyika kwa ajili ya kuchukua nafasi ya zile zilizozeeka na kufa au kwa ajili ya kukarabati majeraha. Saratani huanza wakati seli katika sehemu mojawapo ya mwili zinapoanza kukua bila kudhibitiwa. Ukuaji wa seli za saratani hutofautiana na ukuaji wa kawaida wa seli za mwili na badala ya kufa pale zinapozeeka huendelea kukua na kuzaa seli nyingine mpya zisizokuwa za kawaida. Seli za saratani pia hushambulia kwa kuingia ndani ya tishu nyigine jambo ambalo halishuhudiwi katika seli za kawaida. Kwa kawaida seli za saratani husambaa katika sehemu nyingine za mwili ambako huko nako huanza kukua na kuunda uvimbe (tumor) mpya na baada ya muda kupita, vimbe hizo huchukua nafasi ya tishu mpya. Kukua kusikodhibitiwa na kusiko kwa kawaida kwa seli na tabia ya kuzishambulia tishu nyingine ndiko husababisha seli za saratani.

Ilivyoenea

Kulingana na sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina idadi ya watu milioni 44.9. Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka watu 100 kati ya 100,000 hugundulika kuwa na saratani. Hii ina maana kuna watu wasiopungua 44,000 hugundulika kuwa na ugonjwa huo kila mwaka nchi nzima. Hadi sasa kuna kituo kimoja kinachotoa tiba ya saratani kwa mionzi nchi nzima ambacho kipo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyopo jijini Dar es Salaam, ingawa muda si mrefu kituo kingine kitafunguliwa katika Hospitali ya Bugando.

Kila mwaka zaidi ya watu milioni 12 hugunduliwa kuwa na saratani ulimwenguni. Asilimia 60 ya jumla wanaougua hutokea Afrika, Asia, Amerika ya Kati na Kusini. Ugonjwa huu huua watu wengi zaidi kuliko jumla ya wote wanaokufa na Ukimwi, malaria na Kifua Kikuu. Watu milioni 8.2 walikufa kwa saratani mwaka 2012.

Sifa zake

Si kila uvimbe ni saratani, bali kuna ya vimbe ambazo si saratani nazo huitwa ‘Beningn Tumors’ mfano Tezi dume(Benign Prostate Hyperplasia). Uvimbe huweza kugawanyika na kukua, pia hutengeneza mirija mipya ya damu ili kujipatia lishe wenyewe, kitendo hiki huitwa ‘Angiogenesis’. Uvimbe huu usiokuwa saratani unaweza kuleta matatizo kama vile kukua zaidi na kuvibana viungo na tishu nyingine mwilini. Uvimbe unaweza kukua na kuingilia mifumo ya umeng’enyaji, fahamu na damu/limfu na huweza kutoa homoni zinazobadili utendaji wa kawaida wa mwili. Ingawa uvimbe usiokuwa saratani unaweza kuwa hatari kwa afya lakini hauwezi kuzishambulia seli nyingine au kusambaa katika viungo vingine mwilini. Vimbe za aina hii mara nyingi hutibika na huwa hazihatarishi maisha.

Hata hivyo, aina zote za saratani zina sifa tatu zinazofanana ambazo ni ukuaji usiodhibitika wa seli, uwezo wa kuvamia na kushambulia tishu nyingine na uwezo wa kusambaa katika viungo vingine mwilini kupitia mishipa ya damu au mikondo ya limfu. Kitendo cha saratani kusambaa mwilini kupitia mkondo wa damu na limfu huitwa ‘Metastasis’.

Aina za saratani

Kuna aina zaidi ya 200 kwa kuzingatia ni kiungo gani cha mwili kimeathirika au eneo la mwili linaloshambuliwa. Baadhi ya saratani huwashambulia zaidi wanawake; mfano saratani ya matiti na kuna baadhi ambazo huwashambilia zaidi wanaume. Baadhi ya saratani huwashambulia watu wa kundi fulani katika jamii kutokana na muundo wao wa maisha au kazi wanazofanya na hali kadhalika kuna baadhi ya saratani zinazoshambilia watoto zaidi kuliko watu wazima mfano ya damu aina ya ‘Lymphoblastic’.

Aina za saratani kulingana na tabia

CARCINOMAS; hii ni saratani ambazo hushambulia viungo mbalimbali vya mwili vilivyo ndani na nje mfano mapafu, matiti na utumbo.

SARCOMAS; hii hupatikana kwenye mifupa, misuli na tishu mbalimbali.

LYMPHOMAS; ni saratani zinazoanza kwenye mikondo na vifundo vya limfu na kwenye tishu za kinga ya mwili.

LEUKEMIAS; huanza ndani ya ute wa mifupa (bone marrow) na kukusanyika kwenye mishipa ya damu.

ADENOMAS; huchomoza kwenye tishu na tezi zinazotoa homoni mbalimbali hasa tezi zilizopo kichwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles