NA GABRIEL MUSHI- DAR ES SALAAM
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameziagiza sekta zote na wadau mbalimbali kushirikiana kwa pamoja kudhibiti viumbe vamizi kwa kuwa sasa ni janga la kitaifa.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana alipozindua kikosi kazi cha wajumbe 17 kitakachotatua changamoto za viumbe hao.
Pia alisema hadi sasa Tanzania ina aina 100 za viumbe hao wanaojulikana ikiwamo magonjwa ya mimea, wadudu, magugu katika maji na nchi kavu, wanyama na miti.
Alisema viumbe hao wakiwamo kunguru ni janga la kiuchumi, kimazingira na kiafya.
“Baadhi ya viumbe hao watu wengi tunawafahamu ni mimea aina ya magugu maji yaliyoenea Ziwa Victoria, Ziwa Jipe na Mto Ugalla,” alisema.
Samia alisema uzoefu katika usimamizi wa viumbe hao katika sekta za maji, wanyamapori, uvuvi, kilimo, misitu na nishati ya maji nchini unaonyesha kuwa endapo hatua za kutatua changamoto hiyo zisipochukuliwa mapema wataendelea kusambaa na kusababisha uharibifu mkubwa.
“Janga hili si la sekta moja. Kama tulifanya makosa huko nyuma kushughulikia jambo hili kila sekta kivyake tangu sasa tuache. Sekta zote na taasisi zifanye kazi kwa pamoja kwa kupeana taarifa na mikakati ya kukabiliana na changamoto hii,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, alisema kuundwa kwa kikosi hicho kulitokana na mapendekezo ya mkutano uliofanyika Arusha Septemba 4, mwaka huu na lilikuwa ni agizo la Samia na waligundua moja ya malalamiko ya wafugaji, wakulima na wavuvi ni kuwapo kwa baadhi ya mimea hiyo katika maeneo yao.
Alisema kikosi hicho kitakachoongozwa na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Ezekiel Mwakalekwa, kitakuwa na hadidu za rejea nane.
“Kwanza ni kukusanya taarifa zote kuhusu viumbe vamizi kama vile magugu, kukusanya taarifa za wananchi wanaozunguka maeneo yaliyoathiriwa, kukusanya taarifa za aina ya viumbe vamizi, idadi na ramani vilipo, kuzichambua kisheria taarifa hizo na kuandaa mpango kazi namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.
“Pia kutoa ushauri na mapendekezo, kuandaa mfumo wa kitaasisi namna ya kupeana taarifa na kubadilishana taarifa na mwisho kushughulikia jambo lolote kuhusu viumbe vamizi,” alisema.
January alisema mpango wa kuandaa kikosi hicho ulitokana na ziara aliyofanya maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na kushuhudia mimea vamizi namna ilivyosambaratisha hifadhi hiyo na kusababisha wanyama kuhama kutafuta malisho.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, alisema uwapo wa viumbe hao unatokana na sababu mbalimbali zikiwamo shughuli za kibinadamu, maendeleo ya mfumo wa usafiri duniani akitolea mfano meli, mizunguko ya wanyama kutoka eneo moja na jingine na mabadiliko ya tabianchi pia huchangia kuleta viumbe wavamizi.