26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Samia agoma kuzindua stendi mpya Kibaha

Na MWANDISHI WETU, KIBAHA

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amekataa kuzindua kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi yanayokwenda mikoani kilichopo Maili Moja Kibaha mkoani Pwani.

Vilevile ametaka ufanyike uchunguzi wa kasoro zilizopo kabla ya kukizindua.

Alitoa uamuzi huo jana baada ya kufika katika kituo hicho ambako alieleza wasiwasi wake kuhusu utekelezaji wa mradi huo ikiwamo kubaini upungufu  mbalimbali.

Makamu wa rais  aliagiza ufanyike uchunguzi ndani ya wiki tatu na baada ya kukamilika atarudi   kukizindua.

Alisema kuna minong’ono kuhusu mradi huo hivyo ni jukumu lake kuibeba na atakapojiridhisha atarudi kwa mara nyingine .

Samia  aliahidi kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, mkurugenzi   na Mkuu wa Mkoawa Pwani  kuzungumzia suala hilo na kutafuta ufumbuzi wa pamoja.

“Msishtuke kwa hili ni kawaida  kuchukua hatua za aina hii   kujiridhisha kwa masilahi ya halmashauri, mkoa na watumiaji pia.

“Serikali ya CCM ni sikivu na tumesikia malalamiko ya wananchi. Tumepata malalamiko kidogo kuhusu stendi hii, serikali ni ya uwazi na ukweli hivyo sitofungua stendi,” alisema Samia.

Alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Jennifer Omolo na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama na wahusika waliohusika kufanikisha mradi huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema  wapo wataalamu wanaohakiki lakini yeye kama ameridhishwa na kazi hiyo.

“Kwani kila kazi ina changamoto za ubinadamu, hasi na chanya, lakini wamejitahidi,” alisema Jafo.

Alisema mradi wa ujenzi wa kituo hicho  umepata msaada wa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia wa dola za Marekani milioni 255, ambao unagusa kwenye miji 18 na kujenga vituo vipya tisa, barabara za miji kwa kiwango cha lami na madaraja makubwa.

Awali,   madereva wa bodaboda, walidai   licha ya ujenzi wa kituo hicho cha kisasa,   bado hakuna sehemu ya kujikinga jambo ambalo litawaleta usumbufu wakati wa mvua na jua kali.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha,  Omolo alisema mradi  wa ujenzi wa kituo hicho umegharimu Sh bilioni 2.9 na   mkandarasi amekwisha kulipwa bilioni 2.7.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles