NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Algeria ‘The Desert Foxes’, Christian Gourcuff, ameukubali uwezo ulioonyeshwa na wachezaji wa Tanzania ‘Taifa Stars’ wakiwemo nyota wa kikosi hicho, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Kauli ya Mfaransa huyo imekuja baada ya Stars kutoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya kikosi chake kwenye mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi.
Licha ya Samatta kufunga moja ya mabao hayo sambamba na Elias Maguli, straika huyo alikosa mabao mengi ya wazi ambayo yangeweza kuipa ushindi Stars.
Gourcuff alisema Stars iliwapa wakati mgumu sana kwenye mchezo huo na walilazimika kukaa na mipira kwa kupiga pasi nyingi ili kuwapunguza makali.
“Najua ubora wa timu hii (Tanzania), nimeangalia baadhi ya mechi zao dhidi ya Malawi na Nigeria Septemba, ni timu nzuri sana, wachezaji wake wanacheza kwa spidi sana kama Samatta (Mbwana), Farid (Maliki) na Ulimwengu (Thomas) ni wachezaji hatari na wa fujo sana pamoja na baadhi ya wachezaji wengine,” alisema.
Kocha huyo ambaye atajiuzulu muda wowote kukinoa kikosi hicho mara baada ya mechi ya marudiano dhidi ya Stars, aliongeza kuwa matokeo waliyopata ugenini ni mazuri kwa upande wao huku akidai wapinzani wao wangeweza kuwafunga mabao mengi kama wangekuwa makini katika mchezo huo.
Timu hizo zinatarajia kurudiana kesho kwenye Uwanja wa Stade Mustapha Tchaker jijini Algiers, mshindi wa jumla wa mchezo huo ataingia moja kwa moja katika hatua ya makundi itakayotoa timu tano bora zitakazofuzu kwa michuano hiyo.