NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga TP Mazembe (DRC), Mbwana Samatta, amejibebesha mzigo baada ya kudai kuwa anataka kuiachia timu hiyo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutimkia Ulaya mwakani.
Samatta aliyeivusha TP Mazembe hadi nusu fainali ya michuano hiyo wikiendi iliyopita kwa kufunga mabao matatu ‘hat trick’ walipoifunga Moghreb Tetouan ya Morocco mabao 5-0, anamalizia mkataba wake kwa matajiri hao Februari mwakani.
Wakati mkataba wake ukiwa ukingoni, tayari mshambuliaji huyo ameweka wazi kuwa hataongeza mkataba mwingine TP Mazembe huku akiwa na mipango ya kutimkia barani Ulaya anapowaniwa na baadhi ya timu kutoka Ligi Kuu Ufaransa, Ubelgiji na Ureno.
Samatta aliliambia MTANZANIA jana kuwa atahakikisha anashirikiana na wachezaji wenzake kuiwezesha Mazembe kutwaa ubingwa huo walioutwaa mara ya mwisho mwaka 2010 na kufika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu kabla ya kufungwa na miamba ya Italia Inter Milan mabao 3-0.
“Mimi kiukweli ningependa niiachie TP Mazembe kombe la haya mashindano makubwa Afrika kwa ngazi za klabu, nitahakikisha nashirikiana na wachezaji wengine kutimiza hilo,” alisema.
Mazembe kwa sasa ina mtihani wa kulitwaa kombe hilo, italazimika kuifunga timu ya Kiarabu kwenye nusu fainali itakapocheza na El Merreikh ya Sudan Septemba 25 na marudiano Oktoba 2 mwaka huu.
Mshambuliaji huyo tegemeo wa Mazembe na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, alinukuliwa na gazeti hili jana akikiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na kocha wa El Merreikh, Diego Garzitto, kuijua vema TP Mazembe aliyoifundisha kwa mafanikio msimu wa 2003-2004 na 2009-2010
Kama TP Mazembe itafuzu mtihani huo kwa kuitoa El Merreikh, kwenye hatua ya fainali itakutana na mshindi wa jumla wa nusu fainali nyingine kati ya Wasudan wengine Al Hilal na U.S.M Alger ya Algeria.