28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Simba, Azam zakabana kileleni

pG 32NA WAANDISHI WETU

TIMU za Yanga, Simba na Azam zimeendeleza wimbi la ushindi na kukabana koo kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kushinda mechi zao za pili mfululizo.

Timu hizo zote zina pointi sita, lakini zinatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Yanga ambao wanatetea ubingwa hadi sasa ipo kileleni ikiwa haijaruhusu bao la kufungwa, ila imeshinda mabao matano hadi sasa, ikifuatiwa na Azam ambayo imeshashinda mabao manne na kuruhusu moja la kufungwa.

Simba inafuata katika nafasi ya tatu, ikiwa imeshinda mabao matatu na kutoruhusu bao, wakati Mtibwa Sugar na Majimaji nazo zina pointi sita katika nafasi ya nne na tano.

Yanga iliyokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, iliifunga Tanzania Prisons mabao 3-0, Simba yenyewe ikalipa kisasi kwa kuichapa ugenini Mgambo JKT mabao 2-0.

Azam nayo iliyokuwa ugenini kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ilizidi kumweka pabaya kocha wa Stand United, Mfaransa, Patrick Liewig baada ya kuwachapa mabao 2-0.

Mkenya Allan Wanga alifungua akaunti ya mabao Azam kwa kuifungia bao la kwanza, kabla ya kiungo, Frank Domayo kufunga la pili kuelekea mwishoni mwa mchezo huo.

Yanga ilianza kwa kasi mchezo huo dhidi ya Prisons ikitaka kupata bao la mapema, lakini kadiri muda ulivyokuwa unakwenda walipungua makali na kuiga mpira wa polepole waliokuwa wakicheza Tanzania Prisons.

Hadi dakika 25 za kwanza zinamalizika timu zote zilionekana kucheza sana katikati ya uwanja na kufanya mashambulizi yasiyokuwa na maana hali iliyopelekea kutopigwa shuti lolote lililolenga lango wala kutoka nje.

Yanga ilicharuka na kufanya shambulizi kali dakika ya 26 langoni mwa Prisons, ambapo mpira uliomponyoka kipa wa maafande hao, Mohamed Yusuf, ulimkuta beki Mbuyu Twite aliyepiga shuti kali lililotinga wavuni.

Kipa wa Prisons, Yusuf alifanya makosa mengine dakika ya 44 baada ya kuokoa vibaya mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na kiungo, Thabani Kamusoko, uliomkuta Amissi Tambwe na kufunga bao la pili kwa kichwa na mpira kwenda mapumziko kwa Yanga kuwa kifua mbele kwa mabao hayo.

Kocha wa Prisons, Salum Mayanga, alifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kumtoa kipa wake aliyepwaya, Yusuf na kuingia Aron Kalambo, kisha akamtoa tena Mohamed Mkopi na kuingia Cosmas Ader.

Mwamuzi wa mchezo huo, Alex Mahagi wa Mwanza, alimuonyesha kadi ya njano Lambert Sibianka wa Prisons kwa kumfanyia madhambi, Deus Kaseke, dakika ya 59 alimpa tena kadi ya njano James Josephat kwa kumkwatua Kamusoko.

Yanga iliyoonekana kuimarika kipindi cha pili, ilipata penalti dakika ya 60 kufuatia James kumkwatua Simon Msuva aliyekuwa anaelekea kufunga, iliyopelekea mwamuzi kumuonyesha beki huyo kadi nyekundu iliyotokana na kadi ya pili ya njano, penalti hiyo ilifungwa vema na Donald Ngoma dakika ya 62 likiwa ni bao lake la pili msimu huu.

Kwa upande wao Wekundu wa Msimbazi Simba, iliyoendeleza kuzitesa timu za Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani msimu huu ikianza kwa kuichapa African Sports bao 1-0 wikiendi iliyopita, kabla ya kuilaza Mgambo JKT na kulipa kisasi cha kufungwa nayo mabao 2-0 msimu uliopita kwenye uwanja huo.

Mabao ya Simba kwenye mchezo huo yalifungwa na Mzimbabwe, Justice Madjavi dakika ya 27, aliyeunganisha krosi ya beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwa kichwa, kabla ya Mganda Hamis Kiiza kufunga bao lake la pili msimu huu dakika ya 73 kwa shuti kali la kiufundi lililomshinda kipa wa Mgambo, Said Abdi.

Kocha wa Simba, Dylan Kerr, alimuingiza kipindi cha pili mshambuliaji wake Msenagal, Pape N’daw kwa kumpa dakika tatu za mwisho za mchezo huo, lakini hakuonyesha lolote la maana hadi mpira huo ulipomalizika.

Matokeo mengine, Ndanda iliutumia vema uwanja wake wa Nangwanda Sijaona kwa kuichapa Coastal Union ya Tanga bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji, Atupele Green, Mtibwa Sugar ikaendeleza wimbi la ushindi kwa kuichapa Toto African mabao 2-1 ugenini katika Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Mkoani Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya City ilirekebisha makosa yake ya kufungwa mchezo wa kwanza kwa kuifunga JKT Ruvu mabao 3-0, yaliyofungwa na Joseph Mahundi, Themi Felix na David Kabole.

Mwadui iliyoanza kwa kuchapwa ugenini, ilirejea kwenye dimba lake la Mwadui Shinyanga na kuipa kichapo cha pili msimu huu African Sports cha mabao 2-0, huku Majimaji iliendeleza wimbi la ushindi kwa ushindi nyumbani kwa kuichapa Kagera Sugar bao 1-0.

 

Vikosi

Yanga: Ally Mustafa, Mbuyu Twite, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Geofrey Mwashiuya (dk 80), Amissi Tambwe/Malimi Busungu (dk84), Donald Ngoma na Deus Kaseke/Salum Telela (dk 66)

Prisons: Mohamed Yusuf/Kalambo (dk 46), Salum Kimenya, Laurian Mpalile, James Josephat (kadi nyekundu dk 61), Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Lambert Sabianka, Juma Seif, Mohamed Mkopi/Ader (dk 47), Boniface Hau na Jeremia Juma.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles