*Walikuwa wakisafirishwa kwenda kwa walaji
*Wataalamu wa afya waelezea madhara ya sumu
LUHAGA MPINA na Gurian Adolf -Nkasi
HALMASHAURI ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imeteketeza tani mbili za samaki waliohifadhiwa kwa kutumia sumu ya kuoshea mifugo aina ya DIP ili wasiharibike wakati wanawasafirisha kuwafikisha sokoni.
Sumu hiyo hutumika kwa kuulia kupe kwenye mifugo huku ikitajwa ni hatari kwa afya za walaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa uteketezaji samaki hao, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Missana Kwangula, alisema kuwa walipata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya mfanyabiashara wa Kijiji cha Kalungu, mwambao mwa Ziwa Tanganyika kuhifadhi samaki kwa kutumia sumu ili wasiweze kuharibika haraka.
Alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, wakishirikiana na TFDA, walikwenda kufanya ukaguzi wa samaki hao na kubaini kuwa wamehifadhiwa kwa kutumia sumu aina ya DIP ya kuulia kupe kwenye mifugo.
Kwangula alisema walimkamata mtuhumiwa huyo ambaye ni Dernest Batupu, na alipohojiwa alikiri kuwahifadhi samaki hao kwa kutumia sumu hiyo ili wasiweze kuharibika haraka kwa sababu anawasafirisha mbali nchini Burundi kwa biashara.
Alisema kuwa mfanyabiashara huyo alikubali kulipa faini ya shilingi milioni moja na samaki hao kuteketezwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Kwangula alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya TFDA namba 30 kifungu kidogo cha kwanza A, B na C ya mwaka 2003 inamtia hatiani mfanyabiashara huyo kwa kutenda kosa hilo na ni lazima afikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Hashimu Mvogogo, alisema kuwa samaki wanaohifadhiwa kwa sumu kama hao wana hatari kubwa kwa afya ya binadamu kwani watumiaji wa samaki hao wanaweza kupata maradhi kama saratani na kuwa wao kama idara ya afya wanaiomba jamii kuendelea kutoa taarifa juu ya wafanyabiashara wenye tabia kama hizo ili kukomesha vitendo hivyo.
Ofisa mazingira wa wilaya hiyo, Mayuma Zilantuzu, alitoa wito kwa jamii kuwa makini juu ya matumizi ya samaki wakavu na kutoa taarifa za haraka pale wanapohisi kuwa samaki wanaotumia huenda wana sumu ili hatua zichukuliwe mara moja.
UDHIBITI WA SAMAKI WENYE SUMU
Machi 12, mwaka huu Serikali ilitekekeza katika dampo la Pugu, Dar es Salaam shehena ya samaki waliotoka China wakiwa kwenye kontena lenye urefu wa futi 40 lililoingizwa nchini kwa njia zinazodaiwa za panya.
Akizungumza baada ya kuteketezwa kwa samaki hao, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alisema baada ya kufanyiwa vipimo, waligundulika kuwa na kiwango kikubwa cha zebaki.
“Wao (wamiliki) walipita kwa njia za panya hadi kufika hapa nchini na baadaye kulitelekeza kontena na kufikia hatua ya kupigwa mnada, ilitubidi kufanya vipimo vya ubora tukabaini kiwango cha zebaki kilikuwa PPB 690 wakati kiwango kinachoruhusiwa ni chini ya PPB 500.
“Sumu nyingine tulizokuta ni DDT 2,4’ ambayo kiwango chake kipo 19.4 wakati kinachotakiwa ni chini ya 10, na Methoxychlor imekutwa kiwango cha 19.8 ilhali kiwango kinachotakiwa ni chini ya 10,” alisema.
Mpina alisema madhara ya sumu hizo yanaonekana baada ya muda mrefu kupita na baadhi ya magonjwa ni saratani, matatizo katika mfumo wa uzazi, kuzaliwa kwa watoto wenye upungufu wa akili na kusababisha vifo.
Alisema kuwa mbali na madhara hayo ya kiafya, samaki hao wanasababisha ushindani usio sawa sokoni na kwenda kupora ajira za Watanzania.
Mpina alisema Sheria ya Uvuvi ya Mwaka 2003 na kanuni zake, zinazuia mtu yeyote kuingiza bidhaa nchini bila kufuata taratibu zilizowekwa hasa mazao ya uvuvi.
Alisema umuhimu wa kusimamia na kufuata sheria ni kulinda haki za walaji na afya zao, rasilimali za uvuvi za nchini zinakuwa endelevu kwa kuvuliwa kwa njia zilizo salama, kulinda ajira za Watanzania na kulinda biashara ya uwekezaji nchini.