LIVERPOOL, ENGLAND
MSHAMBULIAJI wa klabu ya Liverpool, Mohamed Salah, yupo hatarini kuukosa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona hatua ya nusu fainali, baada ya kuumia kichwa juzi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Newcastle United.
Mchezo huo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa St James’ Park, ulimalizika kwa Liverpool kushinda mabao 3-2, huku mchezo huo ukiwa na ushindani wa hali ya juu.
Mshambuliaji huyo raia wa nchini Misri, alipata tatizo hilo la kuumia kichwa baada ya kugongana na Martin Dubravka na kumfanya mchezaji huyo atolewe uwanjani huku akiwa amebebwa kwenye machela.
Nafasi yake ilikuja kuchukuliwa na Divock Origi ambaye aliweza kuifungia timu yake bao la ushindi katika dakika ya 86, huku zikiwa zimesalia dakika nne mchezo huo kumalizika.
Salah alionekana kupoteza fahamu kwa muda na ndipo mwamuzi aliamua kusimamisha mchezo kwa ajili ya mchezaji huyo kutibiwa na klabu kutolewa nje. Wakati anatolewa nje, mashabiki wa pande zote mbili walisimama na kumpigia makofi.
Kutokana na hali hiyo, mashabiki wa Liverpool wamekuwa na wasiwasi juu ya mchezaji huyo kuonekana akiwa na kikosi hicho kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Barcelona na mchezo mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya Wolves mwishoni mwa wiki hii.
Hadi sasa hakuna taarifa yoyote kutoka kwa madaktari juu ya hatima ya mchezaji huyo kwamba atakuwa nje ya uwanja kwa muda gani, lakini baada ya mchezo huo kumalizika, Salah alionekana akiweza kutembea mwenyewe akielekea nje ya uwanja huo.
Katika mchezo huo wa kesho, Liverpool wanahitaji ushindi wa mabao 4-0 ili kuweza kusonga mbele hatua ya fainali au wapate ushindi wa mabao 3-0 ili waingie kwenye changamoto za mikwaju ya penalti.
Liverpool watakuwa nyumbani, lakini Barcelona wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na ubora wa wachezaji wao.