29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SAFARI YA KWA LISSU, MKUTANO YAMWEKA SHEIKH PONDA MAHABUSU SAA 32

Na AGATHA CHARLES

KATIBU wa Jumuiya ya Kiislamu na Msemaji wa Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa Ponda ambaye alikuwa akishikiliwa kwa takribani saa 32 na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, baada ya kujisalimisha mwenyewe juzi ameachiwa kwa dhamana.

Sheikh Ponda aliachiwa jana jioni baada ya kufika kituoni hapo Ijumaa saa 3:00 asubuhi.

MTANZANIA Jumapili lilishuhudia akitoka katika viunga vya kituo hicho cha polisi, saa 17:27 jioni.

Sheikh Ponda alitoka akiwa ameambatana na Wakili Kilindo na watu wengine wawili.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili nje ya kituo hicho cha polisi, Wakili Kilindo alisema alipigiwa simu na mpelelezi akimweleza kuwa walikuwa wakisubiriwa wao ili dhamana itoke.

Kilindo ambaye gazeti hili lilimshuhudia akifika kituoni hapo saa 16:45 jioni, alisema baada ya simu hiyo, aliwapigia simu wadhamini ili wakutane kituoni hapo na kuanza kushughulikia dhamana hiyo.

“Mpelelezi alinitaarifu anatusubiri kwa ajili ya dhamana, tumeshughulikia tukiwa na wadhamini watatu, wawili watumishi wa umma mwingine binafsi, lakini amedhaminiwa na wadhamini wawili  ambao ni watumishi wa umma, hivyo kuanzia sasa yuko nje kwa dhamana,” alisema Kilindo.

Alisema polisi waliwataarifu kuwa bado wanaendelea na upelelezi hivyo Sheikh Ponda anatakiwa kuripoti kesho (Jumatatu) muda wowote kuanzia saa 3 asubuhi.

Akizungumzia eneo walilomhoji Sheikh Ponda, Kilindo alisema ni kuhusu safari yake aliyokwenda kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu pamoja na mkutano wake na waandishi wa habari.

Alisema katika mahojiano hayo, Sheikh Ponda alikiri kuwa video, sauti na taarifa yake kwa vyombo vya habari ni vyake na palipokuwa na mapungufu katika mahojiano hayo alielezea ilivyokuwa.

Kilindo alisema Sheikh Ponda ameachiwa baada ya juzi jioni polisi kumchukua na kwenda naye nyumbani kwake kwa ajili ya kumpekua.

DHAMANA ILIVYOSUMBUA

Awali kulikuwa na taarifa za kukanganya kuhusu dhamana ya Sheikh Ponda na kwamba ilielezwa kuwa ilishindikana hadi kesho.

Akizungumza jana kabla ya kupata muito wa simu uliomtaka kwenda kushughulikia dhamana, Kilindo alisema baada ya juzi kushindikana kumtoa Sheikh Ponda kwa dhamana, walitakiwa kurudi jana saa 4:00 asubuhi.

Kilindo alisema hata hivyo walivyofika hapo waliambiwa kuwa haitawezekana kupata dhamana kwa kuwa haikuwa siku ya kazi, kwani ni kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere na ni mwisho wa wiki.

“Tulifika leo (jana) saa 3 asubuhi, tukaingia ofisi namba 13 ili kuzungumzia suala la dhamana kwani walitutaka tuje leo (jana) saa 4 ili kushughulikia, lakini tulivyoongea nao wakasema ni Jumamosi, halafu ni sikukuu, tulikuwa na wadhamini wote na kila kitu kilikuwa tayari,” alisema Kilindo.

Kilindo alisema baada ya majibu hayo mawakili hao waliondoka eneo hilo na kukubaliana kurudi tena saa 7 mchana ili kuendelea na mchakato wa kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kupata dhamana.

MTANZANIA Jumapili ambalo lilipiga kambi katika eneo hilo, ilipofika saa 12:45 mchana, Wakili Kilindi alituma ujumbe kuwa atachelewa kufika kituoni hapo hivyo kumtaka mwandishi amtafute Wakili Juma Nassoro.

Gazeti hili lilimtafuta Wakili Nassoro ambaye alijibu kwa ujumbe mfupi kuwa jitihada za kumpatia dhamana Sheikh Ponda zilishindikana baada ya polisi kuwataka kufanya hivyo kesho.

“Taarifa ni kwamba, Sheikh (Ponda) hakudhaminiwa. Tumepewa taarifa kuwa kwa kuwa leo (jana) ni sikukuu na pia ni wikiendi, hawawezi kutoa dhamana hadi Jumatatu,” alisema Nassoro.

Alisema mahojiano kati ya wapelelezi na Sheikh Ponda yalikuwa yamekamilika na kwamba hata utaratibu wa dhamana ulikuwa tayari.

“Lakini kila kitu kilichokuwa kinahitajika kwa dhamana kilikuwa tayari na mahojiano yamekamilika. Kwa hiyo tunasubiri Jumatatu Inshaallah,” alisema Nassoro.

Mapema jana, Wakili mwingine wa Ponda, Profesa Saffari, alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu licha ya kusema kuwa dhamana ilikuwa ikishughulikiwa, alitaja moja ya masharti kuwa ni mdhamini ambaye ni mfanyakazi wa Serikali.

Ilipofika saa 9:38 mchana, gazeti hili lilimpigia Wakili Kilindo ambaye alisema polisi walimpigia simu kuwa wako tayari kutoa dhamana hivyo aliwasiliana na wadhamani kwa nia ya kwenda kumdhamini.

Itakumbukwa kuwa Alhamisi wiki hii, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alimtaka Sheikh Ponda kujisalimisha polisi ndani ya siku tatu baada ya kudaiwa kutoa lugha za uchochezi, kukejeli shughuli za Serikali na makosa mengine ya jinai.

Hilo lilielezwa kutokea alipofanya mkutano na waandishi wa habari Jumatano wiki hii na kuelezea mazungumzo aliyofanya na Lissu, baada ya kumtembelea katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakotibiwa kutokana na kupata majeraha ya risasi alizopigwa Septemba 7, mwaka huu nyumbani kwake mjini Dodoma.

Polisi walivamia mkutano wa Sheikh Ponda katika hoteli moja iliyopo Kariakoo kwa nia ya kumkamata, lakini hawakufanikiwa badala yake wakaondoka na baadhi ya waandishi baada ya kuwakataza kutotoka ndani ya ukumbi huo hadi watakapompata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles