24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

SADC watakiwa kupambana na ugaidi, utakatishaji fedha haramu

MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

NCHI za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),  zimeshauriwa kuunganisha nguvu zao kupambana na changamoto ya utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa makundi ya kigaidi zinazotishia usalama na kuharibu uchumi wa nchi hizo  .

Ushauri huo umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mwenyekiti wa Maafisa Wandamizi wa Hazina wa SADC, Doto James wakati akifungua kikao cha maofisa waandamizi  wa Hazina  na Benki Kuu wa nchi wanachama wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Akizungumza katika kikao hicho, James ambaye ni Mwenyekiti wa kikao hicho kitakachofanyika kwa siku mbili, alisema kuwa changamoto hiyo imesababisha baadhi ya nchi wanachama kuingia katika orodha ya nchi zilizo kwenye athari ya kuingia kwenye vikwazo vya kimataifa kwa kushindwa kutimiza vigezo na masharti ya Kikosi cha Masuala ya Fedha, hali iyonaweza kuathiri malengo ya jumuiya ya kuvutia uwekezaji.

“Pamoja na mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana kwa miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi wanachama zimeendelea kukabiliana na changamoto nyingine katika sekta za uchumi ikiwemo ukuaji mdogo wa uchumi, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti na hii changamoto mpya ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona,” alisema James

Alisema kuwa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji, pamoja na mambo mengine, wanajukumu la kusimamia itifaki ya Fedha na Uwekezaji katika Jumuiya ya SADC kwa lengo la kuhakikisha Sera na Maamuzi ya Baraza la Mawaziri wa SADC kwenye masuala yanaohusu Fedha na Uwekezaji vinatekelezwa.

“Ili kukabiliana na athari hizo, ni vema nchi wanachama kutumia mifumo ya kitaasisi katika kutafuta njia mbadala zenye ubunifu ili kuharakisha hatua za kuimarisha uchumi ndani ya jumuiya yetu, ni matumaini yangu kuwa kikao hiki ni njia muafaka katika kujadili changamoto za kiuchumi na kutoa mapendekezo ya kitaalam yatakayowasilishwa katika mikutano ya kamati ya mawaziri wa fedha na uwekezaji na magavana wa benki kuu kama ilivyoanishwa katika ajenda za mikutano hiyo,” alisema James.

Alizitaja ajenda nyingine watakazo jadili na kutoa mapendekezo kuwa ni kupitia  taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita  wa kamati ya mawaziri wa fedha na uwekezaji uliofanyika Windhoek, Namibia Julai mwaka jana, kupokea na kujadili taarifa ya hatua iliyofikiwa ya namna uendeshaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC  na kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maandalizi ya Miradi ya Maendeleo wa SADC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles