26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu tano zilizomtumbua Kificho Z’bar

kifichoNA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

SABABU tano zimetajwa kumng’oa aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi visiwani Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, katika kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea wa nafasi ya uspika ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana katika Ofisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, Zanzibar, ambao uliwajumuisha wajumbe 72, Kificho alijikuta akiambulia kura 11 dhidi ya Zubeir Ali Maulid, aliyepata kura 55.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), CCM na baadhi ya wanasiasa visiwani humo, zimezitaja sababu hizo kuwa ni kuchoka kwa mwanasiasa huyo kutokana na umri mkubwa.

Kificho, ambaye amekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi tangu mwaka 1995, sababu nyingine inayodaiwa kukwaza ushindi wake ni hatua yake iliyotafsiriwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba ya kupendekeza muundo wa serikali tatu.

Katika mapendekezo hayo ambayo yalizua mjadala mkubwa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba lililoketi mwaka 2014 na kusababisha upepo mbaya kuvuma ndani ya chama chake kiasi cha yeye mwenyewe kuyakana na kudai Jaji Warioba alimlisha maneno, Kificho alipendekeza Zanzibar na Tanganyika kuwa na mamlaka huru.

Pamoja na Kificho kuonekana kama msaliti ndani ya chama chake na hata alipolitambua na kuweka sawa sawa mambo, akijinasibu kama spika mzoefu baada ya Chifu Adam Sapi Mkwawa, akihudumu katika nafasi hiyo kwa takribani miaka 19 wakati huo, huku akisema hana jeuri ya kusaliti sera za chama chake, bado utetezi huo unaonekana kutomsaidia.

Baadhi ya watu waliozungumza na MTANZANIA Jumamosi, licha ya kumsifu Kificho kwa busara na hekima, lakini wanasema ameponzwa pia na wimbi la mabadiliko ambapo amelaumiwa kutokuwa na kasi ya kuridhisha katika utendaji wake.

Sababu nyingine ni matatizo ya kiafya na ubadhirifu wa fedha ndani ya Baraza hilo, ambao anadaiwa aliufumbia macho.

Kwa matokeo hayo ya sasa, ni wazi Maulid ndiye atakuwa Spika mpya wa Baraza la Wawakilishi baada ya CCM kushinda katika majimbo yote katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na kikao hicho ilieleza kuwa majina yaliyoyapokea ni pamoja na la Kificho mwenyewe, Maulid na Jaji Mstaafu Janet Sekeole, aliyeambulia kura 4, huku mbili zikiharibika.

Kificho ameliongoza Baraza la Wawakilishi kwa miaka 20 tangu alipochaguliwa kushika nafasi hiyo mwaka 1995.

Maulid, aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Kwamtipura  na kushika nafasi  ya Mwenyekiti wa Bunge, atakuwa Spika wa nne tangu kuasisiwa kwa muhimili huo wa tatu wa dola.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Maulid alisema anakabiliwa na changamoto kubwa kukiongoza chombo ambacho kwake yeye ni nafasi mpya.

“Najua nina kazi ngumu ya kusimamia chombo hiki, lakini Mungu atanisaidia pamoja uzoefu wangu nilioupata nikiwa mwenyekiti wa Bunge,” alisema Maulid.

Kwa upande wake Kificho, alisema ameyapokea vizuri matokeo ya nafasi hiyo na hana shaka nayo, kwakuwa katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa.

Alisema yuko tayari kutoa ushirikiano wa aina yoyote ambao utahitajika katika kuendesha chombo hicho.

“Wala haina shaka, ni sisi kwa sisi, kwanini nisitoe ushirikiano wa kuendesha chombo chetu,” alihoji Kificho.

Baraza hilo ambalo ndilo chombo cha kutoa uamuzi visiwani humo, viongozi ambao waliwahi kuongoza ni pamoja na Idrisa Abdulwakil Nombe, ambaye alikuwa rais wa awamu ya nne Zanzibar, ndiye aliyekuwa spika wa mwanzo na kufuatiwa na Ali Khamis, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa vyama vingi 1995.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles