Na LEONARD MANG’OHA
-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetaja sababu nane za kufuta safari za ndege za Shirika la Fastjet Tanzania na kuipa notisi ya siku 28 kujieleza kwanini wasifutiwe leseni ya kuendesha biashara hiyo nchini.
Wakati TCAA ikieleza hayo, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo na mwanahisa mkubwa wa Fastjet Tanzania, alipotafutwa kuzungumzia hali hiyo alisema yupo kwenye kikao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari, alitaja sababu hizo kuwa ni kutokuwa na ndege baada ya moja kati ya mbili zilizosajiliwa nchini kuharibika na kupelekwa nje ya nchi kwa matengenezo, huku moja ikizuiwa na mamlaka hiyo.
Ndege hiyo ilizuiwa baada ya kampuni iliyowakodishia Fastjet kuitaka irudishwe kwa kile walichodai kuwa inafanya kazi bila wao kupata chochote.
Alisema kutokana na uamuzi huo wa mkodishaji kutaka arejeshewe ndege yake, alilazimika kuizuia kama ambavyo sheria ya usafiri wa anga inavyoelekeza.
Johari alisema ndege ambayo imesajiliwa nchini, kwa sasa wameizuia hadi hapo madeni ya kampuni hiyo yatakapolipwa.
Alisema mmoja wa taasisi zinazolidai shirika hilo ni pamoja na TCAA ambayo inadai zaidi ya Sh bilioni 1.413.
Johari alisema baada ya kampuni hiyo kukosa ndege ililazimika kuazima ndege nyingine moja kutoka Afrika Kusini ili iendelee kutoa huduma nchini.
Hata hivyo alisema ndege hiyo pia imezuiwa na mamlaka hiyo tangu juzi baada ya kubainika kuwa ni mbovu.
Alitaja sababu nyingine ya kutoa notisi hiyo ni kampuni hiyo kutokuwa na Meneja Uwajibikaji ambaye ni lazima awe mtaalamu wa masuala ya kiufundi ya ndege.
Sababu nyingine ni kushindwa kuwasilisha andiko linaloonesha kubadilishwa umiliki kutoka kwa mmiliki wa awali ambayo ni kampuni kutoka nchini Uingereza kwenda kwa wafanyabiashara wazawa.
Alisema andiko hilo pia lilitakiwa kuelezea mikakati waliyojiwekea ili kuhakikisha shirika linajiendesha bila kutetereka.
“Wale wamiliki yaani kampuni ya Fastjet plc ya Uingereza ambayo ndiyo ilikuwa strategic investor’ (mwekezaji mkubwa) alisitisha utoaji fedha kwa shirika hilo na kulikabidhi kwa Watanzania ambalo ni jambo zuri.
“Lakini baada ya mabadiliko hayo shirika limetetereka kwa kiasi kikubwa uwezi wake wa kifedha na kushindwa kukidhi masharti ya kile cheti cha uthibitisho na leseni ya biashara.
“Kimsingi baada ya mabadiliko hayo tuliwataka watuletee andiko jipya litakalotafsiri nini kinaendelea ndani ya Fastjet. Kimsingi tuliandikiwa barua kutaarifiwa kuwa kuna mabadiliko, lakini tunahitaji andiko kwamba hao wamiliki wazawa ni kina nani na wana uwezo gani wa kifedha.
“Pamoja na kuangalia masuala ya kifedha pia tunahitaji kujua mkakati wa jinsi shirika litakavyojiendesha bila kutetereka na kuhakikisha masharti ya leseni yanatekelezwa, kwa hiyo tulitaka wafanye hivyo na mpaka sasa hawajafanya hivyo” alisema Johari.
Alisema kutokana na hali hiyo TCAA imeipa kampuni hiyo notisi ya siku 28 ya nia wa kusitisha shughuli za kampuni hiyo nchini na kuitaka kutekeleza masharti ya barua waliyoandikiwa Desemba 9 wakitakiwa kuwasilisha andiko linaloonesha kubadilishwa umiliki na mikakati waliyojiwekea ili kuhakikisha inajiendesha bila kutetereka.
Pia kampuni hiyo imetakiwa kusitisha mara moja mauzo ya tiketi kwa wateja wake ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza pamoja na kuwarudishia fedha abiria wote waliokata tiketi au kuwatafutia nafasi za safari katika mashirika mengine ya ndege.
“Wahakikishe wanalipa madeni kwa wadau wao wote wanaowadai na wawasilishe kwa mamlaka hiyo mpango mkakati unaoeleza kwanini wasifutiwe leseni.
“Lakini kama watafutwa wahakikishe maslahi yote ya wafanyakazi wao yanazingatiwa kabla ya kusitisha rasmi shughuli zao hapa nchini” alisema Johari.
Hivi karibuni Masha kupitia kwa Ofisa Uhusiano na Masoko wa Fastjet, Lucy Mbogoro, alitangaza kununua asilimia 64 ya hisa za kampuni hiyo, hivyo kuongeza hisa zake kufikia asilimia 68 kutoka asilimia nne alizokuwa akimiliki awali.
Ununuzi wa hisa hizo ulitajwa kuwa ni sehemu ya mpango wa kuboresha shirika hilo, kuelekea katika mikakati mipya ya kuboresha huduma za shirika hilo.
Inadaiwa kuwa Masha ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet alinunua asilimia 17 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na kampuni mama ya Fastjet PLC ya Afrika Kusini na asilimia 47 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na wawekezaji wazawa, ikiwa ni mpango wa kuifanya kampuni hiyo imilikiwe moja kwa moja na Watanzania.