Na JUDITH NYANGE-MWANZA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kukutwa na kete 32 za dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni heroine, kilo mbili na nusu za bangi na misokoto 75.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema watuhumiwa hao walikamatwa Februari 22, mwaka huu saa nne asubuhi maeneo ya katikati ya jiji na wote wakiwa ni wakazi wa Nyamagana.
Msangi alisema kabla ya kuwakamata watuhumiwa hao walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu uwepo wao na walianza kuwafuatilia.
“Watuhumiwa tuliowakamata ni Mago Ailaa (29) mkazi wa Mabatini, Emmanuel Marco (24) mkazi wa Bugarika, Josiah Leornad (30) mkazi wa Kirumba, mwanafunzi Allan Marwa (19), Fikiri Msafiri (36), Izack Anderson (31) mkazi wa Igogo, na Omari Ally(27) mkazi wa Mabatini, hao wote wanashikiliwa na polisi kwa kosa la kupatikana wakiwa na dawa za kulevya zinadhodhaniwa kuwa ni heroine zikiwa kete 32, bangi kilo moja na nusu na misokoto 75,” alisema Msangi.
Alisema polisi inaendelea kuwafanyia mahojiano ili kubaini mtandao wa watu wanaoshirikiana nao katika biashara hiyo na uchunguzi utakapokamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.
Alitoa wito kwa wakazi wote wa Mwanza kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa za watumiaji, wauzaji na wasafirishaji wa dawa ya kulevya ili waweze kudhibitiwa.