Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Viongozi na wanachama mbalimbali wa CCM wakiwamo John Ryoba na Ashura Ditopile wamejitokeza kuchangia ujenzi wa nyumba ya katibu wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam inayojengwa Kigamboni.
Ryoba ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni inayojihusisha na utengenezaji wa madirisha na milango ya Wahenga Alluminium ameahidi kuchangia Sh milioni 4.8 wakati Ditopile ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Tawi la Mwasonga amechangia Sh milioni 2 kukamilisha ujenzi huo.
Wanachama hao wamechangia ujenzi huo Oktoba 22,2022 wakati wa uwekaji jiwe la msingi uliofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, ambao pia umeenda sambamba na kuhamasisha watu kuchangia kumalizia sehemu iliyobaki.
“Gharama za milango na madirisha tumeelezwa kwamba ni Sh milioni 9.6, mimi nitachangia nusu yaani asilimia 50 ambayo ni Sh milioni 4.8.
“Sijawahi kujiuliza CCM itanifanyia nini ila nimekuwa najiuliza nitaifanyia nini CCM, nitakuwa sehemu ya historia ya ujenzi wa nyumba hii…tuko tayari kuhakikisha tunakisaidia chama chetu ili kitimize malengo yake,” amesema Ryoba.
Naye Ditopile, amesema “Nipo tayari kutumika kukipambania chama changu, nafanya jitihada hizi kumuunga mkono Mwenyekiti wetu wa Taifa, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Awali, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Adam Ngalawa, amesema ujenzi huo ulianza Juni mwaka huu na mpaka sasa Sh milioni 90 zimetumika.
“Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Mkoa iliyochaguliwa mwaka 2017 hadi 2022 iliazimia ifikapo Desemba 2022 wakamilishe nyumba ili katibu wa mkoa atakayekuwepo ahamie,” amesema Ngalawa.
Kwa upande wake Chongolo amewapongeza viongozi na wanachama kwa kujitoa na kuwataka wajitahidi kukamilisha ujenzi huo haraka.
“Hatuhitaji kusubiri mwezi wa kumi na mbili, kwa Dar es Salaam mkoa ambao una wagombea wa NEC zaidi ya 500 kwenye viti 15 mnaniangusha…speed (kasi) bado ndogo,” amesema Chongolo.
Wengine waliochangia ujenzi huo ni pamoja na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Ojambi Masaburi, Mbunge wa Afrika Mashariki, Abubakar Kachwamba, Hawa Ghasia, Dk. Sebastian Ndege, George Mtambalike, Stella Walingozi, Beatrice Edward, Francis Nanai na makatibu muhtasi kutoka ofisi ya chama ya mkoa.