25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Makatibu CCM mtegoni

Na Norah Damian, Mtanzania Digital

Ni mtego! ndivyo unavyoweza kusema baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kusema watachukua hatua dhidi ya watendaji wanaoshindwa kusimamia mali za chama.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, akikata utepe wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba ya katibu wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam inayojengwa Kigamboni.

Mwaka 2017 chama hicho kiliunda tume iliyokuwa na jukumu la kufuatilia mali za chama kote nchini na baada ya kukabidhiwa ripoti pamoja na mambo mengine kilielekeza zitafutwe nyaraka za kisheria za umiliki wa baadhi ya maeneo.

Akizungumza Oktoba 22,2022 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba ya katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam na jengo la CCM Wilaya ya Kigamboni, Chongolo, amesema kasi ya kutafuta nyaraka za kisheria za umiliki wa maeneo ya chama imepungua.

“Inasikitisha kuona mali ambazo tumezimiliki kwa miaka mingi mtu anajitokeza na kusema hapa kwangu, wenye mali ambao ni chama ngazi husika wanatakiwa kusimamia wapo, wamekaa kimya na baadhi wameacha na kuona si sehemu ya wajibu wao…tutakapoanza kuchukua hatua zitaelekezwa kwa mtendaji wa eneo husika,” amesema Chongolo.

Katika hatua nyingine Chongolo amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaoendeleza rushwa katika uchaguzi na kusababisha wenye dhamira ya kweli ya uongozi kukosa nafasi.

“Chama hiki kina watu wazuri wa kuwa viongozi, tatizo ni baadhi yetu kutengeneza miundombinu haramu ya kuwadhibiti watu wazuri kupata uongozi.

“Tutapitia kila jina, tutapitia maelezo binafsi ya kila mgombea na tutajiridhisha ili tupate viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuendeleza utumishi wa chama chetu mbele.

“Vikao vitakavyoenda kuketi Dodoma vitatenda haki, vitafanya kazi bila upendeleo, wale mtakaobakia msitengeneze nongwa, chama kina nafasi nyingi msipate shida…usipotosha leo utatosha kesho,” amesema Chongolo.

Kuhusu ujenzi huo Chongolo amewapongeza viongozi na wanachama kwa kujitoa na kuwataka wajitahidi kukamilisha haraka.

Ujenzi wa nyumba ya katibu wa mkoa ulianza Juni mwaka huu na mpaka sasa Sh milioni 90 zimetumika na wanatarajia itakamilika Desemba mwaka huu.

Kwa upande jengo la CCM Kigamboni, Katibu wa CCM Wilaya ya Kigamboni, Stanley Mkandawile, amesema ujenzi ulianza mwaka 2020 na mpaka sasa fedha zilizotumika ni Sh milioni 190.7 na kwamba zinahitajika Sh milioni 95.3 kuukamilisha.

Katika hafla hiyo Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile, amemuomba Chongolo kuweka msukumo kwenye Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ili waweze kupata barabara kabla ya 2025.

“Tunaomba pia tuangalie upya tozo za daraja, watu wanasema Kigamboni unaingia kwa fedha unatoka kwa fedha,” amesema Dk. Ndungulile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles