Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
JESHI la Polisi visiwani Zanzibar, limesema litamchukulia hatua za kinidhamu ofisa wake mwenyewe cheo cha Sajenti ambaye alionekana hivi karibuni akipokea rushwa kutoka kwa raia wa kigeni.
Hatua hiyo, imekuja baada ya picha za video kusambaa katika mitandao ya kijamii, zinazomwonyesha askari huyo akipokea fedha ambazo hadi sasa hazijajulikana kiwango chake kutoka kwa raia huyo wa kigeni, ambaye alikuwa na kosa la kutofunga mkanda.
Katika video hiyo, raia huyo anaokana kutoa fedha na kumkabidhi askari huyo huku akiahidi kumsaidia ili asikamatwe mbele ya safari.
Tukio hilo lilitokea eneo la Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ingawa askari huyo alitaja eneo la Mahonda akionyesha nia ovu ya kutenda kosa hilo bila kujijua kama anachukuliwa video.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame alisema jeshi hilo linampongeza raia huyo wa kigeni kwa kutoa taarifa hiyo.
“Jeshi la polisi linachukua nafasi hii kulaani kosa hili, licha ya kua ni kosa la jinai linalifedhehesha jeshi na kulitia doa kutokana na dhamana kubwa lililokabidhiwa,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za jeshi hilo, tayari limeanza uchunguzi mara moja na kwamba litachukua hatua zinazostahili.
Kutokana na hali hiyo, Kamishina Hamdani amewataka wamiliki wa makampuni ya simu za mikononi kufufua mfumo wa upigaji simu kutumia namba za dharura ambazo ni 111 na 112 ili kuwarahisishia wananchi kutoa taarifa.