
Na Muhamed Khamis (UoI), ZANZIBAR
BODI ya udhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), imesema haimtambui Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho.
Imesema pia kwamba haimtambui kama mwanachama wa kawaida hasa baada ya kufukuzwa rasmi uanachama na Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini CUF, Abdallah Khatau alipozungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana.
Alisema bodi hiyo imepuuza wito wa Profesa Lipumba alioutangaza kutaka kuitishwa kikao cha wajumbe wa bodi ya udhamini kwa vile hana mamlaka hayo kwa mujibu wa katiba ya CUF.
“Lipumba kwa sasa si mwenyekiti tena wa CUF na pia si mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa hivyo tumeamua kupuzia wito wake aliotoa jana (juzi),’’alisema Khatau.
Alisema bodi ya uadhamini ya chama hicho itaendelea kuwajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama kama inavyotakiwa na Ibara ya 98(5) ya katiba ya chama ambalo ndilo linaloiteua bodi na litaheshimu uamuzi wote utakaofikiwa.
Alisema bodi itahakikisha inachukua hatua za sheria kwa mujibu wa uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(3) na 98(4) kurejesha chini ya dhamana yake mali zote za chama zilizovamiwa, kuporwa na kuhodhiwa na Profesa Lipumba na aliloliita genge lake likiwamo jengo la Ofisi Kuu ya chama hicho lililopo Buguruni Dar es Salaam.
Alisema bodi hiyo itachukua hatua za sheria kwa uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(4) dhidi ya Ibrahim Lipumba kwa kumtaka alipe gharama na hasara zote alizozisababisha kwa kuvamia Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa wa chama uliofanyika Agosti 21, mwaka huu.