Na JANETH MUSHI-ARUSHA
MAHAKAMA ya Rufani nchini inatarajia kuanza kikao chake na kusikiliza mashauri 45, ikiwamo la kugombea nyumba kati ya aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Kamishna Godfrey Nzowa na Kamanda Mstaafu wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.
Kikao hicho kilichopangwa kuanza Septemba 24, mwaka huu hadi Oktoba 12 mwaka huu, kinatarajiwa kuongozwa na Jaji Bethuel Mmilla, akisaidiana na Majaji Richard Mziray, Sivangilwa Mwangesi na Mwanaisha Kwariko, wote wa Mahakama ya Rufani nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Bernard Mpepo, alisema kati ya mashauri hayo 45, Rufaa za jinai ziko 18, maombi ya jinai yako mawili, rufaa za madai ziko tano na maombi ya madai yako 20.
“Kikao cha Mahakama ya Rufani kitaanza jijini hapa wakati vikao vingine vikiendelea mkoani Mwanza na Dar es Salaam na hiki cha hapa Arusha kitaongozwa na Mwenyekiti, Jaji Mmilla,” alisema.
Katika rufani hiyo namba 124 ya mwaka 2017, maofisa hao wawili waandamizi wa Jeshi la Polisi hapa nchini, wanagombea nyumba ya serikali iliyopo eneo la Uzunguni, jijini Arusha.
Aidha, nyumba hiyo ni moja ya zile walizokuwa wakiishi watumishi wa umma katika uongozi wa awamu ya tatu uliokuwa chini ya Rais Benjamin Mkapa na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambazo ziliuzwa kwa wafanyakazi wa serikalini.
Nzowa anapinga Kova na wenzake kuuziwa nyumba hiyo, ambayo awali alikuwa akiishi (Nzowa) wakati alipokuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO).
Nyumba hiyo aliuziwa Kamishna Kova wakati akiwa tayari amehama mkoani hapa na wakati nyumba hiyo inauzwa Nzowa alikuwa bado ni RCO Arusha, huku akiishi ndani ya nyumba hiyo na familia yake kabla ya kuhamishiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ambapo aliendelea na wadhifa huo.
Awali Februari 26, mwaka 2016, Mahakama hiyo iliondoa rufaa hiyo ya madai baada ya Mahakama kukubali pingamizi lililowasilishwa na Wakili wa Serikali, Sylvester Mwakitalu, kwa niaba ya mjibu Rufani wa pili ambaye ni Wakala wa Majengo (TBA), aliyeomba kesi ifutwe kutokana na kufunguliwa nje ya muda.
Akitoa uamuzi huo jijini hapa, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu, alisema rufani hiyo iliondolewa kwa sababu ilikuwa imefunguliwa nje ya muda kama sheria inavyotaka.
“Baada ya kupitia hoja za pande zote, Mahakama iliamua kuiondoa na mleta maombi (Nzowa) atatakiwa kuwalipa gharama za kesi wajibu maombi (Kova na TBA), kwani sheria inataka Rufaa kuwasilishwa siku 60 baada ya kuweka kusudio la kukata rufaa,” alisema Naibu Msajili Mkwizu.
Hata hivyo, katika uamuzi huo, Naibu Msajili Mkwizu alisema bado mleta maombi Nzowa anayo nafasi nyingine ya kuandaa upya rufaa yake na kuiwasilisha mahakamani hapo tena.
Kabla ya uamuzi huo kuliibuka mvutano wa kisheria kwa pande zote juu ya siku 60 za kukata rufaa mbele ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Jaji Mbarouk Mbarouk, Jaji Mussa Kipenka na Jaji Benard Luanda.
Mjibu maombi wa pili ambaye ni Wakala wa Majengo nchini (TBA), kupitia kwa Mawakili wake aliiomba Mahakama hiyo kutupilia mbali shauri hilo, kutokana na kupelekwa mahakamani likiwa nje ya muda, hoja iliyoungwa mkono na Wakili wa Kova.
Akijenga hoja za upande wao, Wakili Kiseria alidai kuwa, Notisi ya kusudio la kukata Rufaa ilitolewa Septemba 23, mwaka 2013, wakati Rufaa hiyo iliwasilishwa Januari 2, Mwaka 2015, zikiwa zimepita siku 60 za kisheria za kuwasilisha rufaa.