RUFAA iliyokatwa na Rais wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) aliyesimamishwa, Sepp Blatter pamoja na Rais wa Vyama vya Soka barani Ulaya ‘Uefa’ Michel Platini, kupinga kusimamishwa kwa siku 90 zimekataliwa na kamati ya rufaa ya shirikisho hilo.
Blatter na Platini walisimamishwa tangu Oktoba mwaka huu na kamati ya maadili ya Fifa kwa muda wa siku 90 kupisha uchunguzi juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili viongozi hao.
Blatter alianza kukumbwa na kashfa hiyo mara baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano Aprili mwaka huu, ambapo viongozi 14 wa shirikisho hilo walifikishwa mahakamani na ndipo rais huyo akatangaza kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo.
Hata hivyo, baada ya muda alidai kuwa yeye ni msafi na hajahusika na masuala ya rushwa kama inavyodaiwa na watu mbalimbali.
Blatter na Platini walikana makosa yao na sasa wanatarajia kukata tena rufaa katika mahakama ya usuluhishi wa michezo (CAS).
Platini yeye anatarajia kuwasilisha utetezi wake katika mahakama hiyo ya michezo ya Cas leo kwa mujibu wa mwanasheria wake, Thibaud d’Ales.
Wakati huo uchaguzi mkuu wa kumtafuta rais wa shirikisho hilo unatarajiwa kufanyika Februari 26 mwakani, huku Platini akiwa ni miongoni mwa wagombea wa nafasi hiyo.