Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Debora Magiligimba, amewataka wanaume wanaonyimwa unyumba kuripoti katika madawati ya jinsia yaliyopo katika vituo vya polisi kwani huo ni ukatili.
Ametoa wito huo wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili yaliyofanyika katika viwanja vya Tabata shule ambapo pia alikabidhi vitambulisho maalumu kwa madereva bodaboda na bajaji ili iwe rahisi kutambulika.
“Kunyimwa unyumba husababisha kupata ukatili wa kisaikolojia yanapotokea hayo nendeni dawati la jinsia mripoti…nasikia mnauliza mnaanzaje wewe njoo tutakusikiliza,” amesema Kamanda Debora.
Aidha amewataka bodaboda hao kujichunguza wao kwa wao ili kuwabaini wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma, Mrakibu wa Polisi Mosi Ndozero, amesema kuna ukatili katika vyombo vya usafiri ndiyo maana walilenga kutoa elimu kwa bodaboda.
“Unamvizia mtoto wa shule kisha unampa lifti au kinamama wa watu mnawapeleka sokoni siku ya pili unamrubuni huo ni ukatili tuache,” amesema Mosi.
Awali Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata Mrakibu wa Polisi, Colle Senkondo, amesema waliamua kuandaa vitambulisho maalumu vya madereva bodaboda na bajaji wa Kata za Tabata, Kimanga na Liwiti ili kudhibiti vitendo vya uhalifu.
“Kulikuwa na matukio mengi yaliyosababisha bodaboda kuchomwa moto na baada ya kufanya uchunguzi tulibaini si wakazi wa Tabata, ndiyo maana tuliamua tuwe na vitambulisho maalumu,” amesema Colle. Mmoja wa madereva bodaboda katika eneo la Tabata Shule, Majaliwa Hamisi, ameomba walindwe pindi wanapotoa taarifa za uhalifu