Na RASHID NCHIMBI – JESHI LA POLISI ARUSHA
Timu ya Taekwondo Polisi Arusha imeahidiwa vifaa vilivyokosekana katika Gym ya mazoezi yao baada ya kutwaa ubingwa wa Nane Nane.
Michuano hiyo imeshirikisha timu 10 tatu zikiwa za kutoka nchini Kenya.
Timu hiyo imechukua ubingwa katika mashinadano yaliyofanyika tarehe 3 na 4 mwezi huu ukumbi wa Triple A kwa kupata Medali 27 kati ya hizo Nane zilikuwa za dhahabu, saba za fedha na 12 za shaba wakati nafasi ya pili na tatu imechukuliwa na Kilifi na Regional za Kenya.
Ahadi hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi mara baada ya kukabidhiwa kombe la ubingwa huo.
“Pamoja na changamoto kadhaa mlitambua umuhimu wa mashindano hayo na mlionyesha uzalendo wa hali ya juu uliosaidia kuwakilisha taifa letu na Jeshi la polisi kwa kupata ubingwa ambao umekuwa fahari yetu sote.
“Hivyo mimi kama mlezi wa timu hii naahidi kuendelea kutoa vifaa vya mazoezi ili liweze kukamika,” amesema Kamanda Ng’anzi.
Kwa upande wake Mwalimu wa timu hiyo, Master Shija Shija alisema ushindi wa timu hiyo ulitokana na nidhamu, kujituma kwa wachezaji lakini pia kufuatilia maelekezo yake.
“Hawa ni askari huwa wanatii na kuheshimu kila wanachoelekezwa lakini pia uungwaji mkono wa Kamanda wa Polisi umekuwa chachu ya ushindi kwani wachezaji wamekuwa na morali ya hali ya juu,” amesema Master Shija.
Kwa upande wake askari wa kike, Edith Msafiri, amesema ana furaha kubwa kushiriki mchezo huo kwa kuwa unamsaidia katika kazi yake kutokana na ujuzi alioupata na anaoendelea kuupata unaomuwezesha kupambana na wahalifu bila hata kulazimika kutumia silaha.
Aidha Kamanda Ng’anzi alisema mbali na kuwepo timu hiyo pia Jeshi la polisi mkoani hapa limeanzisha, Programu ya kushirikisha askari wote kila ijumaa ili kila mmoja ashiriki katika mchezo anaoutaka kama vile riadha, mpira wa miguu, mpira wa Pete, kunyanyua vyuma na mingine mingi ili afya zao ziweze kuimarika.