LONDON, ENGLAND
NAHODHA wa Timu ya Taifa ya England, Wayne Rooney, baada ya kuachwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo dhidi ya Slovenia, amedai kuwa bado ana nafasi ya kuitumikia England.
Rooney, mwenye umri wa miaka 30, katika mchezo wa awali wa kundi F wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2018, ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Wembley dhidi ya Malta, mchezaji huyo alionekana kuzomewa na mashabiki, japokuwa England ilishinda mabao 2-0.
Hata hivyo, kocha wa timu hiyo, Gareth Southgate, alimkingia kifua mchezaji huyo na kudai kwamba bado alionesha kiwango kizuri, lakini katika mchezo dhidi ya Slovenia, nahodha huyo aliwekwa benchi.
Hali ya kuwekwa benchi kwa mchezaji huyo imewapa watu maswali mengi, huku wakidai kwamba, safari ya mchezaji huyo kuitumikia timu hiyo imefikia mwisho, japokuwa mwenyewe amedai kuwa atahakikisha anafanya vizuri ili kupata namba ya kudumu hadi pale atakapotangaza kustaafu soka la timu ya taifa ifikapo 2018.
“Bado nina nafasi ya kuitumikia England, japokuwa nimewekwa benchi, nitahakikisha ninapambana kurudisha ubora wangu ili niweze kulitumikia taifa katika michuano ya Kombe la Dunia 2018,” alisema Rooney.
Kocha Southgate amesisitiza kuwa ameamua kuachana na nahodha huyo katika mchezo dhidi ya Slovenia, si kwamba ameshuka kiwango chake, ila aliamua kufanya hivyo ikiwa ni mbinu ya mchezo huo.
Nafasi ya Rooney katika uongozi ndani ya uwanja ilichukuliwa na msaidizi wake, Jordan Henderson, lakini Rooney anaamini kuwa bado nafasi yake ipo pale pale.
Hii ni mara ya kwanza kwa miaka 13 sasa Rooney kuwa katika wachezaji wa akiba katika kikosi cha timu ya taifa kuwania kufuzu.
“Nimefanya maamuzi sahihi ya kumuacha Rooney benchi, nilianza kwa kuangalia michezo ya Slovenia iliyopita jinsi wanavyocheza, na nikaangalia nini tunakihitaji katika mchezo huo na ndiyo maana tukaachana na mchezaji huyo.
“Zote zilikuwa ni mbinu za mchezo na kila mmoja alilijua hilo, kwa kuwa tuliweka wazi mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini hii haimaanishi kwamba Rooney kwa sasa si nahodha tena, ataendelea kuwa nahodha hadi pale nitakapokuwa nje ya timu hii,” alisema Southgate.
Hata hivyo, Rooney amedai kuwa huu ni wakati mgumu kwake kwa kuwekwa benchi, lakini amesema yote ni mipango ya kocha.
Rooney kwa sasa ni mfungaji bora wa kihistoria wa England, akiwa na jumla ya mabao 53, akifuatiwa na Sir Bobby Charlton, ambaye alifunga jumla ya mabao 49. Pia ndiye mchezaji wa pili kuichezea mechi nyingi nchi yake, akiwa amecheza mechi 117 nyuma ya kipa Peter Shilton, aliyecheza mechi 125.