27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JPM awapa kiwewe vigogo

magu*Walishawasili Simiyu na mashangingi yao kwa ajili ya sherehe

*Walikuwa wamelipwa posho watakiwa kuzirejesha

 

Na Mwandishi Wetu

RAIS Dk. John Magufuli, amezua kizaazaa kwa viongozi wa Serikali waliokuwa wamewasilia mkoani Simiyu kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru zinazofanyika kesho.

Rais Magufuli amegiza viongozi wote wa Serikali waliokuwa wamealikwa katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kutohudhuria sherehe hizo, huku akiwataka waliokuwa wamelipwa posho za kujikimu na safari kwa ajili ya sherehe hiyo wazirejeshe.

Wakati agizo hilo linatoka jana, tayari baadhi ya wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya walishawasili mjini Bariadi, ambapo wametakiwa kurudi katika vituo vyao vya kazi.

Sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru huadhimishwa Oktoba 14, sanjari na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu JK Nyerere ambapo mwaka zinafanyikia Bariadi mkoani Simiyu.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ilieleza kuwa Rais Dk. Magufuli ametoa agizo hilo, ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.

“Viongozi wote wa Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitakazofanyika Oktoba 14, 2016 katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.

“Viongozi waliotajwa wanatakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na wakuu wote wa mikoa, wakuu wote wa wilaya, wakurugenzi wote wa mamlaka za serikali za mitaa.

“Wengine ni mameya na wenyeviti wote wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya pamoja na watumishi ambao huandamana nao wakiwamo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Kilele cha sherehe za mbio za Mwenge wa Uhuru huenda sambamba na maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14,1999, London Uingereza.

Kutokana na hali hiyo, agizo hilo limewataka viongozi wote wa mikoa na wilaya kubaki maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.

Licha ya hali hiyo, Rais Dk. Magufuli, ameagiza wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.

Hata hivyo, Dk. Magufuli ameelekeza kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na wilaya zake pamoja na wananchi wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru kesho.

Katika sherehe hizo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

 

Viongozi wahaha

Mpaka jana, wakurugenzi  kutoka halmashauri za  majiji, miji, manispaa na wilaya mbalimbali 52, walikuwa wamewasili mjini Bariadi mkoani Simiyu, kwa ajili ya kuhudhuria  sherehe hizo.

Akizungumza baada ya agizo hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenister Mhagama  alikazia agizo hilo kwa kusema viongozi wote waliotajwa katika agizo la Rais, wanapaswa kurejesha posho ambazo walichukua.

“Kama mmelisikia vyema agizo la Rais limewataja viongozi wanaopaswa kurejesha posho na kutoshiriki sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa…sisi ambao hatukutajwa mfano mawaziri, naibu waziri,taasisi za umma  tutaendelea na shughuli hizi,” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga akizungumza na MTANZANIA alisema akiwa ofisa mstaafu wa  Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amepokea maelekezo ya Rais.

“Unajua nilikuja Simiyu  kwa ajili ya kongamano la vijana ambalo limemalizika, naweza kusema kazi iliyonileta nimemaliza. Nilikuja kujifunza zaidi kwa wenzetu hawa kuhusu walivyoweza kuanzisha miradi yao kwa vijana,” alisema.

Akizungumzia suala la urejeshaji wa posho, alisema haina shida watalitekeleza, pia iwapo litamhusu hata yeye aliyeenda kwa lengo la kujifunza katika kongomano hilo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai tayari suala hilo limezungumzwa na Waziri Mhagama.

“Siwezi kuongea tena maana jambo hili limekwishatolewa ufafanuzi na waziri ambaye ni mkuu wangu, naomba waandishi chukueni maelezo ya waziri,” alisema.

 

JPM na matukio

 

Novemba 23, mwaka jana Rais wa Dk. John Magufuli, alitangaza kufuta sherehe za miaka 54 ya  Uhuru kwa mwaka jana ambazo hufanyika Desemba 9  kila mwaka.

Aliagiza siku hiyo itumike kufanya usafi kwa kila mwananchi na fedha za maandalizi ya sherehe hizo Sh bilioni nne  aliagiza zijenge barabara ya Mwenge-Morocco, Dar es Salaam.

Alisema ni aibu kwa taifa kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru huku taifa likikabiliwa na   kipindupindu ambacho kwa kiasi kikubwa kinasababishwa na uchafu.

Aliwaagiza watendaji wote wa halmashauri na manispaa nchini kuhakikisha wanatayarisha vifaa vya kufanyia usafi  kila mwananchi aweze kushiriki.

Novemba 26, mwaka jana  Rais Dk. John Magufuli alisimamisha  maadhimisho ya Siku ya Ukimwi kitaifa ambayo yalikuwa yafanyike mkoani Singida ambayo kilele chake hufanyika kila Desemba mosi.

Rais aliagiza fedha zote ambazo zilitengwa na serikali   na wahisani mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho hayo zielekezwe kununua dawa kwa ajili ya waathirika wa Ukimwi na  vitendanishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles