29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

ROMA MKATOLIKI, STAMINA WAACHA SIMULIZI FIESTA MUSOMA

 Na MWANDISHI WETU

TAMASHA la Tigo Fiesta ni burudani ya kipekee ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki, ambalo hufanyika kila mwaka, likihusisha mikoa mbalimbali ya Tanzania.

 

 

Tamasha hili la muziki limekuwa na mvuto wa kipekee, kutokana na kuhusisha wasanii mbalimbali wanaopendwa na mashabiki kutokana na kufanya vizuri katika nyimbo zao wanazofanya.

 

Kwa mwaka huu, Tigo Fiesta ikiwa na kauli mbiu ya ‘Tumekusoma’, ilizinduliwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, huku msanii Ali Kiba, anayetamba na wimbo wake wa Seduce Me, ukiwapagawisha vilivyo wakazi wa jiji hilo.

 

Tamasha hilo juzi likahamia katika Uwanja wa Karume, mjini Musoma, huku mashabiki wa burudani wakifurika kuwaona wasanii mbalimbali wakiimba nyimbo wanazozipenda.

 

Licha ya mikoa hiyo, tamasha la Tigo Fiesta pia litawafikia mashabiki wa mikoa ya Mwanza, Tabora na Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam.

 

Wakazi wa Musoma ilikuwa zamu yao kuwaona wasanii wakali wakitoa burudani, kwa hakika wamefurahia uhondo kutokana na mwaka jana kulikosa.

 

Tamasha lilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk. Charles Mlingwa, ambaye alisema hiyo ni fursa ya pekee kwa tamasha hilo kubwa kwa kupewa upendeleo wa kuwa mkoa wa pili baada ya Arusha.

 

“Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Tigo na Clouds Media kwa kutuletea fursa mkoani kwetu, najua wakazi wa Musoma mmefaidika sana kwenye biashara mbalimbali, naomba niwahakikishie mtaburudika na mtaondoka salama kwa ulinzi tulioweka,” alisema Mlingwa.

 

Ndipo burudani ilipoanza na wasanii ambao watabaki katika simulizi ya wakazi wa Musoma ni Roma Mkatoliki na Stamina (Rostam), ambao walilibeba tamasha hilo la Tigo Fiesta walipopanda jukwaani kwa pamoja na kuimba wimbo wao mpya uitwao ‘Huku au Kule’, ambao uliibua shangwe na nderemo katika uwanja huo.

 

Roma Mkatoliki, ambaye anatamba na wimbo wake wa Zimbabwe, kupanda kwake jukwaani na kuimba pamoja na mkali mwenzake, Stamina, ilikuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Musoma waliofurika katika Uwanja huo wa Karume.

 

Wasanii hao kwa hakika waliacha simulizi ya kipekee kutokana na kulimudu vyema jukwaa wakiimba wimbo huo, kwa maana nyingine Roma na Stamina hawakuwaacha salama wakazi wa Musoma kutokana na kuimba huku wakifuatisha wimbo huo kwa shangwe.

 

 

Wasanii wengine ambao pia walikuwamo katika kunogesha tamasha hilo katika uwanja huo ni pamoja na Nandy, Ditto, Ben Pol na Jux.

 

Pia alikuwamo Saida Karoli, Joh Makini, Darassa, Mr Blue, Fid Q, Chege Chigunda, Shilole, Dulla Makabila, Adam Mchomvu, Weusi, Coyo na Future JNL.

 

Mmoja wa mashabiki waliohudhuria tamasha hilo, Michael Joseph, mkazi wa Tarime, alisema aliamua kuchanga fedha yake ili ajionee wasanii mbalimbali katika tamasha la Tigo Fiesta.

 

“Kwa kweli sikutaka kusubiri nisimuliwe, nilianza kudunduliza fedha yangu wiki mbili kabla ya tamasha na nimefurahi kuona wasanii mbalimbali,” alisema.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Tigo Kanda ya Ziwa, Edgar Mapande, alisema Tigo imeamua kudhamini tamasha la Tigo Fiesta mwaka huu ili kuendeleza na kukuza vipaji vya wasanii wa ndani, lakini pia kuwaletea wateja wao burudani.

 

“Lengo letu ni kuona wateja wetu wanafurahia burudani, lakini pia kukuza vipaji vya wasanii wetu na kurudisha kwa jamii kile tunachopata,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles