29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

ROMA MKATOLIKI ATEKWA NYARA STUDIO

Na WAANDISHI WETU


WASANII wa hip hop, Ibrahim Mussa maarufu kama Roma Mkatoliki, Monii Central Zone, Bin Laden na Imma ambaye ni mfanyakazi wa mama mzazi wa mmiliki wa studio za Tongwe Records iliyopo Masaki, Dar es Salaam, J Murder, hawajulikani walipo baada ya jana kudaiwa kuvamiwa na kutekwa na watu wasiojulikana.

Uvamizi huo ambao umezua taharuki, unadaiwa kufanyika jana saa 1:30 usiku.

Kukamatwa kwa wasanii hao,  kumetafsiriwa kuwa ni  mwendelezo wa tukio lililomkuta msanii Emanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego, ambaye  wiki mbili zilizopita alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro na kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam kabla hajaachiwa kwa amri ya Rais Dk. John Magufuli.

Ingawa haijajulikana sababu za kukamatwa kwa akina Roma, kwa upande wake Ney wa Mitego alikamatwa kwa sababu ya kutoa wimbo ‘Wapo’, uliotafsiriwa kuwa na maneno makali.

 Mmiliki wa studio za Tongwe Records, J Murder, alipohojiwa na redio Ebony FM, alisema baada ya uvamizi huo wasanii hao na mfanyakazi huyo hawajulikani walipo na hafahamu kisa cha tukio hilo.

“Sijui kisa ni nini kwa sababu sikuwepo studio, ila ninachojua ni kwamba walikuja watu na gari aina ya Noah, walimuhoji Roma baada ya hapo waliwahoji na watu wengine, kisha waliingia ndani ya studio wakachukua baadhi ya vifaa vya studio na wakaondoka na wasanii wangu, wakiwamo Roma, Monii, Bin Laden na mfanyakazi wa mama yangu anaitwa Imma na hatujui hadi leo wapo wapi ingawa namba zao zinaita bila kupokewa,” alieleza J Murder.

Zaidi J Murder alisema wakati uvamizi huo unafanyika, hakukuwa na ulinzi wowote katika studio hiyo isipokuwa wasanii hao waliotekwa na majirani ambao ni mashabiki wake.

“Jana usiku baada ya kutokea tukio hilo nilikwenda kutoa ripoti Polisi Oysterbay, kwa sasa nawaomba mashabiki tuwaombee ndugu zetu wawe salama maana hatujui waliko, mali si tatizo kwa sababu zinanunulika, tatizo ni watu wangu kwanza, maana huwezi kununua roho ya mtu,” alisema mmiliki huyo.

 

MKE WA ROMA

Mke wa Roma, Nancy (Mama Ivan) amewaomba watu wanaojua alipo mume wake wasaidie kumpata.

Alisema hadi jana alikuwa hafahamu wala hakuwa na taarifa zozote juu ya mahali alipo mume wake.

Nancy alisema mara ya mwisho aliwasiliana nae juzi saa 12 jioni na alimweleza kuwa anakwenda Tongwe Records kwa kazi zake za kila siku.

Alisema baada ya hapo hakumpata tena katika simu jambo ambalo alilichukulia kuwa ni hali ya kawaida na kuamua kulala.

“Lakini saa sita au saba usiku nilipokea simu kutoka kwa rafiki mmoja wa Roma, aliniuliza upo na Roma? Nikamwambia hapana, ameelekea Tongwe, akaniambia kuna taarifa kwenye mitandao zinaendelea, nami nikaingia kwenye mitandao nikapata taarifa kama wengine wanavyopata,’’ alieleza.

Nancy alisema baada ya hapo, aliwatafuta watu wa kumsaidia kuendelea kumtafuta vituo mbalimbali vya polisi, lakini hawakuwaona.

“Sina ninachokijua jitihada zangu za kutafuta kwenye vituo vya polisi vyote nimemaliza sijui alipo na hakuwa akitafutwa, alikuwa akiishi kama kawaida, kila siku anatoka anakwenda Tongwe anarudi salama, lakini jana hakurudi na polisi walisema watafuatilia ili nao wajue yuko wapi, hivyo kama kuna mtu anasikia, anajua alipo atusaidie maana mimi hadi saa hizi sijui chochote,’’ alisema kwa masikitiko Nancy.

 

BUNGENI DODOMA

Tukio hilo lilimlazimisha Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Chadema) jana kuomba mwongozo wa Spika.

Kutokana na ombi hilo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliiagiza Serikali kuchukua hatua haraka ili kufahamu ukweli wa suala hilo ili kulipatia ufumbuzi.

Sugu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, aliomba mwongozo huo kwa Spika muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu bungeni.

“Mheshimiwa Spika, saa moja usiku jana (juzi), watu wenye silaha wakiwa kwenye gari Toyota Noah walivamia Studio ya Tongwe Records na kuwateka watu wanne, akiwamo msanii Roma Mkatoliki na hadi sasa hawajulikani walipo.

“Mheshimiwa Spika, tukio hili linafanana na lile la kukamatwa kwa msanii Ney wa Mitego… Mheshimiwa Spika, inavyoonekana sasa matukio haya ya kutumia silaha ya kuwatishia watu yanazidi kushamiri katika nchi yetu, tulishuhudia Redio Clouds kuvamiwa na silaha nzito na tukashuhudia Nape (Mbunge wa Mtama) kutishiwa kwa bastola, ni nani anawatuma watu hawa kufanya hivi?” alihoji Sugu.

Katika majibu yake, Ndugai alisema:  “Katika hili niseme tu Serikali ilifuatilie haraka na kulipatia ufumbuzi maana siwezi kutoa ufafanuzi zaidi, maana ndio ninalisikia hapa kwako kwa mara ya kwanza.”

 

POLISI DAR ES SALAAM

Kamanda wa Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alipoulizwa kwa simu kuhusu tukio la kuvamiwa na kutekwa kwa wasanii hao, alimtaka mwandishi ampigie baada ya nusu saa akidai kwamba alikuwa kwenye mkutano.

“Nipigie baada ya nusu saa, nipo kwenye mkutano,’’ alijibu Kamanda Sirro.

Alipotafutwa baada ya muda huo, alihoji kila aliloulizwa kuhusu tukio hilo kisha  akakata simu.

 

TAMKO LA CHADEMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa ofisa habari wake, Tumaini Makene, kimepokea kwa masikitiko tukio hilo huku kikidai kuwa kinalichukulia kwa uzito mkubwa.

Makene alisema kuwa tukio hilo ni mwendelezo wa vitisho na mashambulizi dhidi ya uhuru wa maoni na kujieleza kutokana na matukio mengine ya namna hiyo kujitokeza siku za hivi karibuni.

Alisema Chadema inalaani vikali tukio hilo na wote waliohusika kulitekeleza na zaidi akilitaka Jeshi la Polisi kutumia uwezo wake kuhakikisha Roma na wenzake wanapatikana ikiwa ni pamoja na kuvikomesha vitendo hivyo.

Pia alitoa wito kwa makundi mbalimbali katika jamii kutambua kuwa vitisho  na mashambulizi dhidi ya haki na uhuru wa wa watu vinavyofanywa kinyume na Katiba vinastahili kupingwa na kukemewa kwa nguvu zote kwani vikiachwa hakuna mtu atakayekuwa salama.

 

Habari hii imeandaliwa na ELIZABETH HOMBO (DODOMA), JESCA NANGAWE NA ESTER MNYIKA (DAR ES SALAAM).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles