ALIYEKUWA kocha wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers, amedai kwamba kwa sasa hana mpango wa kuzifundisha klabu kubwa tano za juu ambazo zinafanya vizuri katika ligi.
Kocha huyo alifukuzwa na Liverpool Oktoba mwaka jana kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo huku nafasi yake ikichukuliwa na Jurgen Klopp ambaye alikuwa anaifundisha Dortmund.
Tangu afukuzwe Rodgers Oktoba mwaka jana hadi leo hii bado hajapata timu ya kuifundisha japokuwa zilijitokeza klabu zaidi ya tano zikimtaka kufanya naye kazi, lakini kocha huyo alikataa na kudai kwamba ni muda wake wa kupumzika hadi majira ya joto mwaka huu.
“Kufundisha timu kubwa ambazo zinafanya vizuri kuna changamoto zake, niliwahi kuifundisha klabu ya Leading na mambo yalikuwa mazuri, nikajiunga na Swansea City nako kulikuwa kuzuri, lakini Liverpool mambo yamekuwa tofauti.
“Baada ya kuondoka Liverpool nimeamua kupumzika kwa muda japokuwa kulikuwa na klabu kubwa ambazo zilikuwa zinanihitaji, lakini nilikataa kujiunga na sina mpango huo wa kuzitumikia klabu ambazo zinafanya vizuri kwa kuwa kuna changamoto zake,” alisema Rodgers.