32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI ZA MADINI ZIPELEKWE BUNGENI, SERIKALI PIA ILIACHE BUNGE

KWA takribani wiki mbili sasa sakata la mchanga wa madini limetawala katika mijadala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kwenye vyombo vya habari.

Msingi wa kuwapo kwa mijadala inayoshuhudiwa sasa ni ripoti ya wataalamu wa sayansi iliyokabidhiwa kwa Rais Dk. John Magufuli mapema wiki iliyopita.

Katika ripoti hiyo, pamoja na mambo mengine, imeonyesha kuwapo kwa uzembe wa baadhi ya watumishi ambao walipewa jukumu la kukagua kiwango cha madini kilichomo kwenye mchanga  kabla ya kusafirishwa na wawekezaji nje ya nchi.

Tangu wataalamu hao watoe ripoti hiyo kumekuwa na kauli mbalimbali kutoka kwa wasomi, watu wa kada tofauti tofauti na wawekezaji, Kampuni ya Acacia ambao wameomba iundwe tume huru ili kubaini ukweli.

Suala hili sasa limeteka mijadala ya Bunge baada tu ya juzi, Wizara ya Nishati na Madini kuwasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/18.

Bunge limetaka lipelekewe ripoti hiyo iliyowasilishwa na wataalamu kwa Rais Magufuli.

Tunadhani ni vyema Rais Magufuli akatekeleza suala hili, hasa baada ya ripoti nyingine za wataalamu wa sheria na uchumi zitakapomaliza majukumu yake na kisha kuwasilisha ripoti zake.

Tunasema hivyo tukiamini kuwa, Bunge ambalo moja ya kazi yake kubwa ni kuisimamia serikali na zaidi kutunga sheria ambazo baadhi yake sasa zinanyooshewa kidole, itakuwa ni muafaka kwao kuangalia kwa mapana makosa yaliyofanyika nyuma ili yaweze kuwekwa sawa.

Baadhi ya sheria ambazo wataalamu wanaamini ndicho kiini cha serikali kupoteza mabilioni ya fedha kama ilivyoainishwa na Kamati ya Rais ni pamoja na ile ya Madini ya mwaka 1998 na ile ya mwaka 2010.

Lakini pia Marekebisho ya Sheria ya Fedha iliyofuta kwa kiasi kikubwa kodi, tozo na ushuru kwa makampuni ya madini na sheria ya uwekezaji Tanzania inayozipa kampuni za nje kinga za kisheria ambazo zote zilipitishwa na Bunge.

Pamoja na kwamba mara zote Bunge na hasa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi wamekuwa wakinyooshewa vidole kwa kupitisha sheria kishabiki pasipo kuangalia maslahi mapana ya Taifa, ni vyema Rais Magufuli akubali ombi lao la kupelekewa ripoti hizo ili watakapozichambua waone matokeo ya ushabiki wao na fedheha waliyoisababishia Taifa hili.

Si hivyo tu, pia tunadhani itawasaidia wabunge, kama si sasa basi wakati mwingine kutimiza wajibu wao katika Taifa hili.

Mbali na hilo, pia tunadhani ni wakati muafaka sasa wa serikali kuliacha Bunge litimize wajibu wake kikatiba wa ibara ya 63 (3) (e) wa kujadili na kuridhia mikataba yote  inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake yanahitaji kuridhiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles