30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Ripoti ya CAG yamweka kikaangoni Mweka Hazina Kishapu

Na Damian Masyenene, Shinyanga

Wiki kadhaa baada ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Dk. Charkes Kichere kuipa hati ya mashaka Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Madiwani wa halmashauri hiyo kwa kauli moja wameazimia kumsimamisha kazi Mweka hazina wa halmashauri hiyo, Deus Ngelanizya kwa kosa la kushindwa kusimamia mapato ya mwaka wa fedhan 2020/2021 na kusababishia halmashauri hiyo kuwa ya mwisho kitaifa kwenye makusanyo ya nusu mwaka.

Madiwani hao wamesema kuwa mweka hazina huyo anapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kusimamishwa kazi kwa makosa ya kuzarau maagizo ya madiwani na kuisababishia halmashauri kupata hati ya mashaka kwa mwaka 2019 /2020, huku Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Mang’era Mang’era akitakiwa kujitathimini utendaji kazi wake wa kazi kwa sababu anajukumu la kufuatilia mipango yote ya halmashauri hiyo.

Maazimio hayo yamefikiwa jana Aprili 21, 2021 kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo baada ya baraza hilo kukaa kama kamati na kujadili juu ya wafanyakazi hao.

Akitangaza maazimio ya madiwani hao, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, William Jijimya ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mondo, amesema wameamua kutoa maazimio hayo kwa sababu wameshindwa kusimamia kikamilifu mapato ya halmashauri hiyo, hali ambayo wameisababishia kupata hati ya mashaka na kuwa ya mwisho kitaifa.

“Tumekuwa tukiwaagiza wasimamie kukusanya mapato ya ndani lakini hawasimamii kikamilifu, hivyo tumeona tuwaadhimie ili wasiendelee kudharau hili litakuwa ni fundisho na kwa watendaji wengine wa halmashauri hii kwani mapato ni roho ya halmashauri hivyo tunatakiwa kuwajibika kila mmoja ili kuhakikisha mapato yanaongezeka,” alisema Jijimya.

Naye Diwani wa Kata ya Mwamalasa, Bushi Mpina alisema wameamua kuwaadhimia watumishi hao kwa sababu hawasimamii fedha kikamilifu, fedha zinaingia lakini hawajui inaenda wapi hivyo wameona ukusanyaji unaofanywa sio sahihi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Jonhson amesema kama inatokea changamoto ya kusababisha hati ya mashaka idara ya fedha ilitakiwa kusaidiwa, kutoa ushauri na kuwa weledi katika suala la mapato, pia unahitajika ushirikiano wa hali ya juu katika kusimamia mapato.

“Kama miongoni mwetu ameadhimiwa mwenzetu kwa changamoto ya kusababisha hati ya mashaka inatakiwa tujitahimini wote, kwani tulitakiwa kuwasaidia idara ya fedha na kuzingatia weledi na taaluma zetu kwa sababu suala la mapato ni letu sote, tunatakiwa tushirikiane ili kuondokana na changamoto hii,” amesema Jonhson.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kengese amesema ni jambo la aibu kuona halmashauri hiyo ina kuwa ya mwisho kitaifa na kupata hati ya mashaka, hivyo watumishi wote wanatakiwa kujituma katika kusimamia mapato na kuongeza vyanzo mbadala kwa ajili ya kuongeza mapato.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga, Lucas Nyanda amewapongeza kwa kusimamia vizuri maendeleo ya wananchi kwa sababu sifa ya kiongozi ni kuonyesha njia, lakini katika kusomeka kwa kupata hati ya mashaka haikutakiwa kufikia hatua hiyo, ni vizuri kutengeneza mazingira mazuri ili mapato yaweze kuongezeka.

“Ni aibu kubwa kwa sisi wanakishapu kupata hati ya mashaka hatutakiwi kufikia hatua hii hivyo kwa hili mliloliadhimia na watumishi wengine watajisimamia, dhamila yetu ni kuendelea kushikamana tunatakiwa kuwa na mazingira mazuri ya kuweza kuongeza kipato chetu,” amesema Nyanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles