Joseph Hiza na Mashirika,
KWA mashabiki wa soka hasa wale wanaofuatilia Ligi Kuu ya England mwaka juzi watakuwa wanakumbuka kiungo mahiri wa Klabu ya Manchester City, Yaya Toure alipogombana na mwajiri wake huyo.
Kisa? Alikasirishwa na kile alichosema mwajiri wake alishindwa kumfanyia hafla ya siku yake ya 31 ya kuzaliwa.
Ni ugomvi, ambao uliripotiwa na vyombo vya habari duniani kipindi hicho.
Hilo lilitokea wakati City ilipokuwa ziarani Falme za Kiarabu, ripoti ambazo hata hivyo zilikanushwa na matajiri hao wa Etihad.
Hebu fikiria, hii ni siku yako ya kuzaliwa. Unaenda kazini hasa katika mahali ambako kuna au kumeanza utamaduni wa kupeana zawadi kwa siku kama hiyo.
Lakini hakuna mtu anayeonekana kukujali licha ya kufahamu umaalumu wa siku hiyo kwako. Utajisikiaje? Hakuna shaka utakata tamaa na kuhisi kutengwa au hisia za upendeleo. Nini kitatokea baada ya hilo? Molari yako ya kazi itashuka.
Hiyo ni hali ambayo Toure aliihisi kipindi kile kwani alisikika akisema wamiliki wa klabu yake walimpuuza na hakukuwa na mtu aliyeshikana naye mikono kumpongeza, akiashiria hakukuwa pia na kitu kama keki.
Lakini Man City ilijibu kwa kutoa picha ya video ya mwanasoka huyo wa kimataifa raia wa Ivory Coast akikabidhiwa keki wakati timu ikiwa safarini kuelekea Abu Dhabi.
Soka ni kazi yake Yaya na mahali pake pa kazi katika Manchester City anayoitumikia.
Hali hiyo haishangazi maana mahali pa kazi kuna tamaduni nyingi zilizo rasmi na zisizo rasmi kama sehemu ya sera au miongozo au kazini humo.
Tamaduni hizi za kupongezana haziishii wakati wa siku za kuzaliwa bali pia wakati wa siku nyingine kama vile linapotokea jambo fulani la furaha ikiwamo kupanda cheo, kutunukiwa tuzo, shahada, kurudi kutoka likizo, kupata mtoto na kadhalika.
Vionjo vyote hivyo hulenga kuchochea hali ya utani, furaha, mshikamano, upendo na moyo wa kufanya kazi miongoni mwa wafanyakazi.
Kupongezana huko hufanyika kwa namna mbalimbali huku vitu vitam tam kama vile biskuti au pipi na hasa keki kutokana na urahisi wake kupatikana pamoja na mazoea vikitumika zaidi.
Wakati mwingine kampuni husika chini ya meneja wake hugawa zawadi hizo kila wiki kwa wafanyakazi wote.
Utakuta wafanyakazi wa kampuni wakipeana zamu au majukumu ya kununua ama kutengeneza keki kwa ajili ya fulani wakati siku yake ya kuzaliwa.
Yaani mfanyakazi ‘A’ anamnunulia au kumtengenezea ‘B’ keki wakati wa siku yake ya kuzaliwa na B anafanya hivyo kwa A inapofika siku yake.Hali kadhalika X na Y.
Keki hizo haziliwi na wawili hao tu bali hugawiwa kwa wengi wa wafanyakazi kama ishara ya kufurahi pamoja.
Utamaduni kama huu umeingia hata hapa Tanzania, ambako utakuta wafanyakazi wakirudishiana fadhila kwa kununuliana au kutengenezeana keki.
Keki hizo hugawiwa kwa wengi wa wafanyakazi, ambao wanaweza kuwa wote waliopo siku husika au idara fulani ama kundi la marafiki kutegemeana na bajeti.
Hata hivyo, licha ya uzuri wa utamaduni kama huu kazini una mabaya yake na moja wapo ni suala la kiafya.
Ni kwa vile kugawana vitu vitamu hutokea mara kwa mara, karibu kila siku, kila wiki au vinginevyo ukizingatia siku kama za kuzaliwa hutofautiana. Leo huyo, kesho yule na keshokutwa mwingine.
Hata hivyo, kwa sababu hiyo, madaktari wa meno wameushutumu utamaduni huu, wakisema unachangia kwa kiasi kikubwa matatizo ya kiafya.
Idara ya afya ya meno nchini Uingereza imesema kuwa watu wanapaswa kupunguza ulaji wa keki, biskuti na pipi makazini kwa sababu vyakula hivyo vinawafanya kunenepa kupitia kiasi mbali ya kuwasababishia afya mbaya ya mdomo.
Profesa Nigel Hunt amesema kuwa wafanyakazi wanahitaji kubadilisha utamaduni wa kazini ili kuweza kupunguza ulaji wa vyakula vyenye sukari.
Amewashauri wafanyakazi kutumia vyakula hivyo kama chakula cha mchana kama si kuviacha kabisa.
Professa Nigel Hunt, Mkuu wa Kitivo cha Upasuaji wa Meno katika Chuo cha Royal College of Surgeons, alisema huenda wasimamizi wa ofisi hizo wanataka kuwazawadia wafanyakazi wao kwa juhudi zao.
Nao wafanyakazi hutaka kusherehekea siku za kuzaliwa au mafanikio mengine, kuleta zawadi ofisini na kadhalika hatua ambazo zinasababisha vyakula vya sukari nyingi kuingia ofisini kwa wingi.
Lakini amesema kuwa hilo linaathiri afya ya wafanyakazi na ni muhimu kufanya uamuzi katika Mwaka Mpya wa kukabiliana na utamaduni wa vyakula vya sukari.
“’Ijapokuwa peremende hizo huenda zikawa na maana, zinachangia unenepaji wa kupitia kiasi pamoja na afya mbaya ya mdomo,”aliongeza.
Tunahitaji kubadili utamaduni katika ofisi zetu ambao unashawishi ulaji wa vyakula vya afya na unawasaidia wafanyakazi kutotumia vyakula vya sukari kama vile, keki, peremende na biskuti.
“Kwa watu wengi mahali pa kazi kwa sasa ni moja ya maeneo makuu ambayo yanaingiza mwilini sukari kwa wingi na hivyo kuchangia janga la sasa la unene na afya mbaya ya mdomo.
“Ni hatari sana kukaa ofisini siku nzima na wakati huo huo kuingiza mwilini mlo usiotakiwa kwa wingi.”
Anaongeza: “Utamaduni wa keki pia unaleta ugumu kwa wale wanaojaribu kupunguza uzito au kutaka kuwa wenye afya njema. Utakuta mtu anafanya mazoezi au anajitahidi kujidhibiti kwa mlo.
“Lakini bahati mbaya anakutana na majaribu mengi akiwa kazini kutokana na wingi wa vitamu anavyovishuhudia vikipitishwa pitishwa kila siku na kushindwa kujizuia.
Kwa sababu hiyo, Prof Hunt anasema kwamba waajiri au waandaaji waache kutoa biskuti au pipi wakati wa mikutano au semina.
“Sisemi kwamba tunahitaji kupiga marufuku utamaduni huu bali tunahitaji kubadilika kwa kuupunguza.
“Wakati watu waapoenda kufanya ununuzi na kununua keki na vitamu vingine wanapaswa kununua angalau kiwango kidogo na kukifanya kitumike wakati wa mlo wa mchana tu.
“Kimsingi wafanyakazi wa ofisini wanapaswa kutafuta njia mbadala kwa kutumia vitu kama matunda, karanga badala ya vitamu tamu. Waajiri wanaojitambua wanapaswa kuepuka vitu hivi wakati wa mikutano,” anasema.