25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU: USAFIRI WA MWENDOKASI KUSUKWA UPYA (2)

Na Bakari Kimwanga-DAR ES SALAAM                |      


UKUSANYAJI wa mapato ni moja ya msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli ambaye kila mara amekuwa akikazia umuhimu wa agizo lake la kuwa na wawekezaji wanaofuata sheria  za nchi.

Aprili 24, mwaka huu wafanyakazi wanaokatisha tiketi katika vituo vya mabasi vya mwendokasi, walifanya mgomo baridi wakishiniza kulipwa mishahara yao.

Mabasi hayo ambayo yanaendeshwa kwa ubia na Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART ), huku mbia mkubwa akiwa Kampuni ya Simon Group katika awamu ya kwanza ya majariobi ya mradi huo.

UDART ni mbia wa Serikali katika mfumo wa PPP na ni haki kwa Serikali kuisaidia kampuni hii yenye lengo la kurejea mikononi mwa wananchi kwa kuuza hisa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).

UPIGAJI WATIKISA

Kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), William Gatambi, mradi huo wakati unaanza mwaka 2016, ulikuwa na abiria 75,000 na kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 200,000.

Alisema kutokana na usumbufu uliojitokeza kwa abiria wanaamini mwekezaji mwingine atapokuja mabasi yote yatakuwa 305.

“Kwa hiyo ndiyo maana tulikuwa tunasema wanasubiri kwa sababu ya upungufu wa mabasi si kwa makusudi, lakini suluhu ya aina hiyo Serikali inaleta mtoa huduma wa pili hivi karibuni ambaye ataleta mabasi ambapo pamoja na yaliyopo yatakuwa mabasi 305 na haya mabasi yataanza kutoa huduma kabla ya mwisho wa mwaka huu,” alisema.

Kutokana na idadi mapato yanatokanayo na abiria ambapo kwa kila safari hulazimika kulipa Sh 650 ukijumlisha kwa idadi hiyo mapato kwa siku yanayokusanywa hufikia Sh milioni 130,000.

MTANZANIA ilifanya uchunguzi kwa zaidi ya miezi mitatu ambapo wakati wa mgomo wa Aprili 24 pamoja na ule wa Mei 16, Serikali imepoteza zaidi ya Sh milioni 300 kutokana na uzembe ambao kwa namna moja au nyingine huenda ukasababishwa na kukosekana kwa usimamizi mzuri kwa waliopewa kazi hiyo.

Katika kile kilichobainika kutumia ‘fursa’ hasa kutokana na mgomo huo baridi,  hasa baada ya kukwama kwa ukatishaji wa tiketi za Kieletroniki, baadhi ya madereva wa magari hayo yanayofanya safari kutoka Kimara-Mbezi walishinda wakikusanya fedha milangoni huku abiria wakipanda bure kwenye vituo vingi vya mabasi hayo.

TIKETI MILANGO

Makusanyo hayo ya fedha milangoni yalifanywa asubuhi ambapo abiria wengi wasiokuwa na kadi maalumu za UDART, walikuwa wakikata tiketi za Kiletroniki chini ya Kampuni ya Maxcom Afrika Plc, ambao kwa sasa wanaonekana kusitisha huduma hiyo.

Tukio kama hilo lilijirudia tena Juni 2 na 3, mwaka huu ambapo mabasi ya mwendokasi yalitoa huduma bure kwa siku ya pili, chanzo cha hali hiyo inadaiwa kuwa ni mgomo wa wahudumu wa kitengo cha tiketi

Hatua hiyo imetokana na wahudumu kugoma kufanyakazi kutokana na kutolipwa malimbikizo ya madeni yao tangu wakiwa chini ya Kampuni ya Maxcom Afrika Plc.

TIKETI ZA VISHINA

Hatua hiyo iliwafanya abiria wanaotumia usafiri huo jijini Dar es Salaam kutoka  sehemu mbalimbali ya jiji kulazimika kusafiri bure baada ya kukosekana mashine za kieletroniki.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa UDA-RT katika hali ya kushangaza ulikuwa ukikatisha tiketi za mabasi hayo kwa njia ya karatasi mithili ya usafiri wa daladala, huku walinzi na maofisa wanaokatisha tiketi hizo wakushindwa kuwazuia abiria na hivyo kuzua vurugu vituoni.

Vituo vilivyokumbwa na vurugu kubwa ni vya Kimara, Korongwe, Kivukoni, Morocco na Gerezani hali iliyowafanya walinzi kushindwa kuwathibiti wananchi waotumia usafiri huo ambapo wengi walipanda bure magari hayo – bila kukata tiketi za mkono za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Vurugu hizo pia zilisababisha magari hayo kujaa kupita kiasi huku katika baadhi ya vituo watu wakionekana kujaa kutokana na uhaba wa magari hayo ambayo kwa muda wa miaka miwili tangu mabasi hayo yalipoanza kutoa huduma hiyo hakuna dalili zozote za uboreshaji wa huduma hiyo.

Kutokana na hekaheka hiyo, pia walifanyakazi waliokuwa wakikatisha tiketi ambao wapo chini ya Kampuni ya UDA-RT nao waliingia kwenye mgomo baridi wa asubuhi huku wengine wakipiga kambi katika ofisi za kampuni hizo zilizopo Jangwani.

ABIRIA WANENA

Mmoja wa abiria wa usafiri huo aliyejitambulisha kwa jina la Thomasi Kilima, aliiambia MTANZANIA kuwa hali hiyo imesababisha shida kwao.

Naye Ramadhan Issa, aliliambia MTANZANIA kuwa tiketi za UDA walizoanza kutumia kwa siku ya jana zinajenga mazingira ya wizi kwani kunakuwwa hakuna udhibiti wa fedha za Serikali.

“Hizi tiketi za UDA nilikuwa naziona usiku pindi unapokata, lakini jana naona ndiyo zimepamba moto. Hata wanaotukatia unaona kuna mazingira ya ujanja sana ikiwemo kukosema udhibiti wa fedha za Serikali na hapa ndipo ulaji unapokuwa, ni vema Serikali iamke sasa na kuliangalia hili kwa jicho la tatu.

“Usafiri huu ni mzuri ila kilichokosekana ni udhibiti na si ajabu tukaja kusikia usafiri huu nao umekufa kama ilivyokuwa UDA ya zamani. Serikali amkeni tiketi hizi ni wizi mtupu,” alisema na kuonya Issa.

MAXCOM  YARUKA

Wakati wakazi wa jiji hilo wakikumbwa na adha hiyo, Kampuni ya Maxcom Afrika (Maxmalipo),  ilitoa taarifa yake na kusema kuwa hawahusiki na utoaji wa huduma ya tiketi za kielektroniki kwenye mradi huo.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma,  Deogratius Lazari ilieleza kuwa kampuni hiyo ni mmoja wa wabia wanaoshiriki kutoa huduma katika mradi huo, kazi ambayo ilianza Mei 16, mwaka 2016 baada ya kuzinduliwa kwa kipindi cha mpito.

Alisema kuanzia Aprili 13, mwaka huu kumekuwa na hali ya sintofahamu katika vituo vya mabasi ya mwendo kasi, ikiwa ni pamoja na uuzwaji wa tiketi za karatasi (za vishina) ambazo hazitolewi kwenye mfumo wa tiketi za kielektroniki ulioidhinishwa na wasimamizi wa mradi huo.

Alisema katika mkataba wao, Maxcom ilihusika kuweka mifumo, rasilimali watu, teknolojia na wasimamizi katika mradi.

Alisema hivi karibuni UDA-RT walitumia nguvu kuwatisha na kuwaondoa wafanyakazi waliokuwa wanatoa huduma ya tiketi za kielektroniki katika vituo vya mabasi ya mwendokasi, bila kufuata taratibu zilizoainishwa kwenye mikataba ya ajira zao.

TTCL WARUKA KIMANGA

Aprili 13, mwaka huu Kampuni ya Usafirisha wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), ilitangaza kumalizika kwa mkataba baina yake na Kampuni ya Maxcom Afrika katika ukataji wa tiketi na kutangaza huduma hiyo itafanywa na Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL).

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa kampuni hiyo, Deus Bugaywa mbele ya waandishi wa habari.

Alisema mabadiliko hayo ni moja ya njia ya kuboresha huduma zao ambapo TTCL kutokana na kuwa na mkongo wa taifa wanaamini wateja wao watapata huduma iliyo bora.

Siku chache baafa ya kutolewa kwa taarifa hiyo na Bugaywa, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), lilisema halihusiki kwa namna yoyote na ukatishaji wa tiketi isipokuwa lina kazi ya kusambaza mawasiliano kupitia mkongo wa Taifa.

UDART WAISHTAKI SERIKALI

Mei 11, mwaka huu, baada ya Serikali kutangaza kupata mwekezaji wa pili wa Mradi wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), hatimaye mwendeshaji wa kwanza wa mradi huo, Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART), alitua mahakamani kuishtaki Serikali.

Uamuzi wa Serikali kutafuta mwekezaji mwingine ulitokana na Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART ), kuonekana kusuasua katika uendeshaji wa mradi huo.

Kesi hiyo, namba 50 ya mwaka 2018, imefunguliwa na Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART), katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, ikipinga kuletwa kwa mwekezaji huyo.

Kampuni ya UDART, ambayo ni kampuni tanzu ya Kampuni ya Simon Group, imefungua kesi hiyo na kupangwa chini ya Jaji Amiri Mruma.

MWEKEZAJI MPYA

Aprili 30, mwaka huu Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Tawaka za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Josephat Kandege, alisema ili kumaliza kero hizo, tayari kandarasi imeshatangazwa na mwendeshaji mpya ameshapatikana.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu, Kandege alisema wanatarajia kuongeza mwendeshaji wa pili ili kuongeza ushindani katika utoaji wa huduma hiyo na kuboresha hali ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.

“Taratibu zimefuatwa na kandarasi imeshatangazwa  na ameshapatikana mmoja anayejiita Emirates kutoka Dubai, nao wataingiza mabasi yao.

“Siwezi kusema ni lini ataanza kuingiza mabasi na kuendesha mradi kwa sababu taratibu za zabuni zipo kwenye ku-award, ila niwahakikishie tunakwenda vizuri… kuna mambo machache  ambayo hayajawa confirmed (thibitishwa). Jambo la msingi ni kuhakikisha tunapata operator (mwendeshaji)  mzuri  ili wananchi wa Dar es Salaam waendelee kuenjoy (kufurahia)  usafiri mzuri.

“Unajua kukiwa na waendeshaji kama wawili au watatu huyu kwanza akisema anapata hasara utamwambia unapata hasara vipi wakati mwenzako wanapata faida?

“Kulikoni akiwa mmoja ndio kama haya yanatokea mara anasitisha huduma, lakini kama asipotoa huduma mwenzake anafanya basi mwananchi anapata huduma,” alisema Kandege.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles